Kushindwa katika maisha hakuji kwa bahati mbaya bali kuna kuja kutokana na tabia zetu ambazo tunazo kila siku kwenye maisha yetu. Tabia hizo kiuhalisia zinaturudisha nyuma sana kimafanikio kama tunazikumbatia.
Kupitia makala haya ya leo nataka nikukumbushe baadhi ya tabia chache tu, na kama tabia hizo utazikumbatia uwe na uhakika unazidi kuukaribisha umaskini ukunyemelee kwenye maisha yako na kukupoteza kabisa.
Inatakiwa kuwa makini sana na tabia hizi ambazo zinaweza zikaingilia uhuru wako wa kifedha na kuweza pengine kukuharibia karibu kila kitu kwenye maisha na kukuacha ukiwa mtupu hauna kitu.
Tabia hizi ni zipi, twende pamoja tuweze kujifunza;-
Tabia 1: Matumizi yako ni makubwa sana.
Kama una matumizi makubwa kwa namna yoyote ile huwezi kukwepa kuishiwa. Inatakiwa matumizi yako uweze kuyabana kiasi cha kwamba yapate nafasi ya kukupa pesa ya ziada. Ni vizuri kuwa na daftari la kumbukumbu litakalokusaidia kutunza kumbukumbu zako za matumizi ili kimatumizi usikengeuke kwa kutumia sana pesa zako hovyo.
Tabia 2: Pesa nyingi unatumia kwenye usafiri.
Iwe matumizi ya nauli za kawaida au matumizi ya gari lako binafsi ila kama pesa zako nyingi unazitumia hovyo kwenye usafiri tu, basi jiandae kuanguka pia kiuchumi. Haiwezekani ikawa karibu muda wako wote ni wewe wa kusafiri tu, halafu ukategemea mambo yako yakaenda sawa. Kuwa makini na matumizi ya pesa unazotumia kwenye usafiri, vinginevyo umaskini unakufuata.
Tabia 3: Unazungukwa na marafiki wabovu.
Marafiki zako wanaokuzunguka ikiwa tabia zao ni mbaya juu ya matumizi ya pesa, basi hata wewe utakuwa ni miongoni mwao. Haitawezekana kwako wewe uweze kukwepa kiunzi hicho hata siku moja ni lazima utakuwa kama rafiki zako tu na sio vinginevyo. Kukwepa hilo unatakiwa kuchagua marafiki makini zaidi kwenye matumizi ya pesa.
Tabia 4: Huweki akiba.
Pengine nikuulize unafikiri, ni kitu gani ambacho kitatokea ikiwa wewe kila aina ya pesa kwako unayoipata unaamua kuitumia. Jibu ni rahisi sana hapo ni utaendelea kushiwa na mwisho wa siku unaukaribisha mwenyewe umaskini. Usijaribu kujiingiza kwenye mtego huu, pesa yoyote unayoipata iwekee akiba hata kama ni kidogo sana, wewe weka akiba.
Tabia 5: Unatawaliwa na matumizi ya starehe.
Hapa utakuta badala ya mtu kuwaza maendeleo, lakini kila pesa unayoipata wewe unawaza ni kwa namna gani utakavyoweza kuifanyia matumizi tena matumizi ya starehe. Hakuna mafanikio yanayokuja kwa nama hiyo kwa kutafuta vitu vya starehe peke yake. Kama uko ‘siriazi’ na kutafuta pesa itafute, la sivyo tabia hii itakuachia janga kubwa sana la umaskini.
No comments:
Post a Comment