SERIKALI
imewaasa viongozi wa dini waeuepuke migogoro ya mara kwa mara katika
Makanisa yao na badala yake waendelee kuwajenga waumini wao wakue kiroho
na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa.
Pia
imesema inawashukuru viongozi wa dini na madhehebu yote ya dini kwa
kuendelea kuiombea nchi amani, mshikamano na utulivu, jambo ambalo
linaongeza chachu kubwa kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
Hayo
yalisemwa Mei 20, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ibada ya
kutawazwa Askofu Dkt. Maimbo Mndolwa wa Dayosisi ya Tanga kuwa Askofu
Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Ibada hiyo imefanyika
katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika
Jijini Dodoma.
“Nawaombeni
wote kwa ujumla wetu, tuendelee kutumia Makanisa yetu kuombea Taifa
hili ili tuendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano”. Watu wa
Mungu ni watu wa Upendo, watu wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu
ni watu wa kiroho”.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa “haitarajiwi kuona watu wa Mungu wakiwa katika
mstari wa mbele kuchochea migogoro, kuvunja amani ya Kanisa na kuongoza
makundi yanayopingana katika kazi ya Bwana”.
Amesema
jukumu la makanisa ni kuwajenga waumini kukua kiroho, na kazi ya
kuwaongoza watu wamjue Mwenyezi Mungu, ambapo amewaomba imani yao iwe
moja na matendo yao yafanane na yale ya Kristo Yesu wanayemuamini.
Waziri
Mkuu amesema kuwa nchi haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi na kijamii
bila kuilinda amani iliyopo, hivyo amewaomba warejee kumbusho la
maandiko Matakatifu katika Waebrania 12:14 “Tatufeni kwa bidii kuwa na
Amani na watu wote”.
Pia
Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi hao na wananchi kwa ujumla
waendelee kuwaombea viongozi wa Tanzania hususani Rais Dkt. John
Magufuli, kuendelea kuwa na afya njema, busara, upendo, hekima katika
kuiongoza nchi yetu.
Waziri
Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli katika ibada hiyo amesema
Serikali inatambua ushirikiano uliopo kati ya madhehebu mbalimbali ya
dini nchini kwa ujumla wake na kwamba ushirikiano huo ni wa kihistoria.
Amesema
mara zote madhehebu ya dini yamekuwa yakisaidiana na Serikali katika
kutoa huduma za elimu, afya, maji na makundi maalum kama vile yatima,
wazee, walemavu, wajane na huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa
Watanzania wote bila ubaguzi wa aina yoyote. “Mambo haya hayawezi
kupatikana nchini bila ya kuwa na amani”.
Kwa upande wake Askofu Dkt. Mndolwa baada ya kutawazwa aliahidi kulitumikia kanisa la Anglikana katika kweli, haki na upendo.
“Naahidi
kwa makini kwamba nitaistahi na kudumisha na kuilinda Imani, haki na
uhuru wa Kanisa la Anglikana Tanzania na kulitumikia katika kweli, haki
na upendo, nisijifanye kuwa bwana juu ya urithi wa Mwenyezi Mungu, bali
katika mambo yote nioneshe kielelezo kwa kundi la Kristo. Mungu
nisaidie,”.
Askofu
Dkt. Mndolwa anashika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Jacob Chimeledya kumaliza muda wake.
Askofu Chimeledya alitawazwa mwaka 2013.
Maaskofu
wengine waliowahi kuongoza kanisa hilo tangu kuasisiwa kwake nchini ni
John Thomas Mhina Sepetu (1970-1978), Askofu Musa Kalemo Kahurananga
(1979-1983), Askofu John Auckland Ramadhani (1984-1997), Askofu Donald
Leo Mtetemela (1998-2008), Askofu Valentino Leonard Mokiwa (2009-2013).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment