RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali kutokana na vifo vingi vya wananchi vikiwemo vingi vya watoto na akina mama kutokana na huduma mbovu za afya, Serikali ina mpango wa kujenga hospitali za wilaya 67 na kukarabati hospitali za mikoa ili kuhakikisha huduma za afya nchini zinawafikia wananchi kwa uhakika ikiwa ili kupunguza vifo hivyo nchini.
Magufuli ameyasema hayo leo mei 2, 2018 Mkoani Iringa wakati akiweka jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo ambapo amesema serikali itaboresha sekta ya Afya hususani vifaa tiba, madawa, miundombinu na wataalam.
“Tumeamua kuweka kipaumbele katika sekta ya afya kwa sababu tumekuwa tukipoteza wakina mama wengi, tumeshaanza kuchukua hatua, tulipoingia madarakani tuliamua kubadilisha bajeti ya wizara ya afya.
“Hospitali hii itakuwa kubwa mno, itakuwa na uwezo wa kufanya upasuaji, vipimo vya X-ray na tiba nyingine kubwa. Kuna hospitali zingine za mkoa haziifikii hii ya Kilolo. Niwaombe viongozi wa wilaya na mkoa tujitahidi tumalize kuijenga ili iwasaidie wananchi wetu, mimi mwenyewe nitaifuatilia. Ninataka pesa itolewe na wakandarasi wajenge usiku na mchana ikamilike haraka.
“Nimuombe Mkurugenzi, uongozi wa wilaya na wa mkoa wa Iringa muanze mchakato wa kuandaa wafanyakazi (madaktari na wahudumu wa afya) ili hospitali hii ya Kilolo itakapokamilika tu, waajiriwe na waanze kufanya kazi mara moja”, amesema Dkt. Magufuli.
Magufuli amewataka Watanzania kujiunga katika Mifuko ya Bima ya Afya ili waweze kunufaika na uboreshaji wa sekta hiyo ya Afya kutokana na kupata uhakika wa kutibiwa kwa gharama nafuu kupitia mifuko hiyo pindi mwanapougua.
No comments:
Post a Comment