Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kusema watu ambao wanasema elimu imeshuka nchini wanakosea kwani kuna sehemu ambazo elimu inaonekana ipo vizuri akitolea mfano wa chuo cha kilimo cha Sokoine University of Agriculture (SUA).
Magufuli amesema hayo leo Mei 7, 2018 akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kusema kuwa watu wasiseme kwa ujumla kushuka kwa elimu ili hali kuna sehemu watu wanafanya vizuri katika elimu, na kudai kuwa wa SUA wameweza kufundisha mpaka Panya na akaelewa hivyo ni wazi kuwa wapo vizuri sana.
"Unajua hata watu ambao wanasema elimu imeshuka sijui kama wamefika hapa kwa sababu wangefika hapa na kumuona Panya anajua bomu liko wapi nadhani asingesema elimu imeshuka, wanamuona Panya amefundishwa mpaka akaelewa eti binadamu ndiyo asielewe, mjue walimu wa hapa wanafundisha mpaka Panya siyo binadamu tu, mpaka anaelewa akinusa hapa kuna kifua kikuu"
Rais Magufuli aliendelea kuzungumzia jambo hilo na kusema kuwa walimu wa SUA na wanafunzi wapo vizuri sana katika masuala ya shule ndiyo maana wanaweza kufanya gunduzi mbalimbali ambazo zinatija na msaada katika maisha ya kila siku.
"Wanafundisha Panya mpaka anatengeneza mapapai mpaka anafanya 'crossbreeding', anafanya papai lianze kuzaa likiwa na miezi mitano badala ya kusubiri miaka mitano halafu linazaa 'production' ya matunda mawili matatu, hizi kazi wamefanya hawa watu yaani hapa kuna vichwa tuache 'generalization' lakini pia lazima tuelewe elimu yetu imetoka wapi, palikuwa na elimu ya UPE aliiacha baba wa taifa kwa sababu hapakuwepo watu wa kwenda kufundisha"
"Nakumbuka baadae likaja suala la kupeleka walimu nafikiri ilikuwa enzi za Mwinyi au Mkapa mtu ukipata 'division zero' kidato cha nne au 'division four' unapelekwa ualimu hayo ndiyo matokeo, tulifanya hivyo kwa sababu ya hali halisi ya wakati huo, tumekuja kwenye awamu iliyopita mimi nimefukuza wanafunzi karibu elfu saba pale UDOM yaani 'four four' wanakwenda kuchukua 'Degree' walipelekwa kwenye awamu ya nne, kwa hiyo ukifuatilia unaweza kujua tumetoka wapi na tunaelekea wapi" alisisitiza Rais Magufuli
Mbali na hilo Rais Magufuli amekiri kuwa katika awamu yake ya tano wamekuja na elimu bure na kusema kuwa huenda baadae ikaja kuwa na madhara ila itasaidia kuondoa ujinga kwa watu wengi ambao walikuwa wakikosa elimu hiyo kwa sababu ya kukosa ada ya kulipa shule.
"Na sisi tumekuja tumeingiza elimu ya karo bure wanafunzi wameongezeka walioingia darasa la kwanza wameongezeka mara mbili zaidi wakawa milioni mbili kutoka milioni moja, hivyo inawezekana hii nayo ikaleta madhara baadaye, mtu mwingine angeweza kusema kwamba tungewaacha tu ili wakawe mambumbumbu waweze kutawalika vizuri kwa hiyo tukaaongeza idadi ya wanafunzi wanaoingia darasa la kwanza"
Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini Mkapa miezi kadhaa iliyopita aliwahi kusikika akisema kuwa kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu ya Tanzania kwa madai kuwa kuna unadhaifu mkubwa na kushukwa kwa kiwango cha elimu ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment