Kocha mkuu wa Ngorongoro Heroes Ammy Ninje, amefunguka sababu za kumwanzisha kwenye benchi mlinda mlango wa timu hiyo na klabu ya Yanga Ramadhani Kabwili.
Ninje amesema Kabwili aliungana na kambi ya timu hiyo akiwa amechelewa hivyo kufanya mazoezi kwa siku moja tu, kitu ambacho kama kocha alikitazama na kuamua kumwanzisha Abdul Twalib ambaye alikuwa kambini muda mrefu.
“Kwenye timu wachezaji unawaangalia mazoezini halafu ndio unapanga timu, sasa Abdul Twalib alifanya vizuri sana mazoezini ingawa alifanya kosa moja la kutoa pasi haraka lakini mazoezini amefanya vizuri sana tofauti na Kabwili ambaye alichelewa kujiunga na kambi'', amesema.
Kabla ya mchezo wa jana ambapo Ngorongoro ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa vijana wa Mali, kulikuwa na tatizo la mawasiliano kati ya Yanga, TFF na Ninje juu ya Kabwili kuungana na kambi ya timu hali iliyopelekea kocha huyo kumwengua kikosini.
Baadae Rais wa Shirikisho la soka nchini Wallace Karia aliingilia kati suala hilo na kuamua Kabwili aungane na kambi ya timu ya taifa baada ya kumaliza majukumu yake ya kuiwakilisha Yanga kimataifa.
No comments:
Post a Comment