Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala limejadili taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kamati tatu ambazo ni kamati ya Fedha, Uchumi na Huduma za jamii pamoja na kamati ya Mipango Miji na Mazingira za Halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwezi January hadi Machi 2018.
Akisoma taarifa ya kudumu ya kamati ya Uchumi na huduma za jamii Kaimu Mwenyekiti, Helen Lyatula amesema kamati yake imesimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali mbalimbali za miradi ya maendeleo ikiwemo kusimamia taaluma na nidhamu katika shule zote za awali na msingi za Serikali na zisizo za Serikali na kutoa muongozo na utaratibu mbalimbali wa kufanikisha malengo waliyoweka kulingana na sera ya elimu.
" Jumla ya walimu 1653 wa shule ya msingi wanatarajia kupandishwa vyeo na madaraja, lakini halmashauri pia imepokea vitabu 100, 904 toka TAMISEMI na kusambaza kwa shule zote msingi," amesema Lyatula.
Amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata bado kumekuwepo na changamoto zinazokabili idara na vitengo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa madai ya likizo hadi sasa jumla ya walimu wa shule za msingi 1837 wanadai kiasi cha Tsh 478,346,684,00, pamoja na ukomo wa bajeti katika utekelezaji shughuli mbalimbali za kilimo, ushirika na umwagiliaji.
Aidha katika Taarifa ya kamati ya fedha na utawala yenyewe imesimamia mapato na matumizi ya Halmashauri ambapo imefanikiwa kukusanya jumla ya Tsh 10,348,333,506 sawa na asilimia 88 ya makisio ya Tsh 11,793,447,388.50 bila kuweka kodi ya majengo ya Tsh 800,000,000.00 ambazo zinakusanywa na Serikali kuu .
Akisoma taarifa hiyo Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo,Waziri Mweneviale amesema katika kipindi cha robo hiyo, halmashauri imefanikiwa kushinda kesi takribani saba ikiwemo kesi na. 54/2003 kati ya Charles Moses dhidi ya halmashauri ya manispaa hiyo ambapo mdai alikuwa akiidai halmashauri kiasi cha Tsh 1,500,000,000 hivyo kwa kipindi hicho kamati imeokoa kiasi hicho cha fedha.
Aidha kamati hiyo imeidhinisha matumizi ya force account kwa ajili ya ujenzi wa ukuta wa pavement katika hospitali ya Mama na Mtoto Chanika kwa gharama ya Tz 183,864,091.20.
Pia amebainisha kuwa kamati hiyo imeweza kusimamia uchangiaji wa mapato ya ndani kwenye miradi ya Maendeleo kwa asilimia 60% na kwamba halmashauri ilichangia jumla ya shilling 3,900,000 kwenye Akaunti ya Maendeleo ikiwa ni sawa na asilimia 80% ya kiasi kilichopangwa kwa kipindi hicho cha January hadi Machi.
Pia baraza hilo limejadili kuhusu kero ya muda mrefu ya Barabara ya Mnyamani iliyopo Buguruni na kusema kuwa itaanza kutengenezwa baada ya mvua kuisha.
Akitoa ufafanuzi wa ujenzi wa barabara hiyo Kaimu Meya wa Ilala Jacbo Kissy amesema barabara ya Mnyamani inatarajia kupata ufumbuzi na kwamba Wakala wa Barabara TARURA ndio wenye mamlaka ya kusimamia barabara zote za halmashauri.
Nae Muhandisi wa Ujenzi Manispaa ya Ilala Justine Magoda amesema ujenzi wa barabara ya Buguruni Mnyamani unatarajia kuanza mara baada mvua za masika kumalizika wakati akijibu swali la Diwani wa Mnyamani Shukuru Dede alipouliza kuhusu kuchelewa ujenzi wa barabara hiyo.
Mhandisi Justine alisema shilingi bilioni 2.5 zinatarajia kutumika katika ujenzi wa Barabara ya Mnyamani Kampuni ya BECCO ndio wamepewa jukumu la kujenga barabara hiyo.
"Ujenzi wa Barabara hii utatumia miezi sita kwisha kwake tunaomba ushirikiano mara baada kuanza kwa ujenzi huu"alisema.Justine.
No comments:
Post a Comment