Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limesema uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari aina ya LandCruiser mali ya Serikali ya Tanzania ndiyo chanzo cha ajali ya gari hilo kugongana na lori na kusababisha vifo vya watu watatu, wawili kujeruhiwa.
Ajali hiyo imetokea jana Mei 21, 2018 katika Kijiji cha Msoga Chalinze Mkoa wa Pwani.
Akizungumza leo Jumanne Mei 22, 2018 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jonathan Shanna amesema watakuwa wakali kwa madereva watakaokiuka sheria za usalama barabara bila kujali wadhifa wao.
Amesema dereva wa gari hilo alihamia upande mwingine wa barabara wakati anayapita magari mengine bila kutazama mbele, hivyo kuligonga lori hilo.
"Sheria za usalama barabarani hazina watu maalumu wa kuzitii, sio kwamba ukiwa dereva wa ofisa wa Serikali basi wewe uende tu hovyo au ukiwa muajiriwa wa Serikali napo ujione mwamba, hata kama ni dereva wangu tutakushughulikia tu,” amesema.
Akisimulia ajali hiyo, amesema watu watatu ambao ni watumishi wa Serikali wakiwa safarini kwenda Dodoma kikazi walifariki dunia katika ajali hiyo.
Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Martin Laurence (39), Zacharia Nalinga (49) na Said Moshi, miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha.
No comments:
Post a Comment