Na Clonel Mwegendao
SERIKALI inafanya tathmini kuhusu fidia ya ardhi na maendelezo yake katika eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya iwapo kutakuwa na utwaaji ardhi wakati wa zoezi la kuimarisha mpaka linaloendelea mkoani Mara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bibi Doroth Mwanyika alisema hayo wakati alipokagua kazi ya uimarishaji mpaka katika eneo la pwani ya Ziwa Victoria mkoani Mara katika kijiji cha Kirongwe kata ya Bukura Wiilayani Rorya.
Amefafanua kuwa Serikali inafanya tahmini hiyo kwa lengo la kuona wananchi waliopo katika eneo huru (buffer zone) iwapo watatakiwa kupisha eneo hilo, itumike njia bora ya kujadiliana nao au kama kuna njia mbadala ya kuwasaidia wananchi hao.
“Kwanza wananchi walioendeleza maeneo ya mipakani walipewa elimu wakati wa zoezi la uhamasishaji lililofanywa na wataalam wetu, wengine wameelewa na kuchukua hatua ya kupisha wakati kazi ya uimarishaji mpaka inaendelea,” alisema Bibi Mwanyika.
Aidha serikali imebainisha kuwa itahakikisha inatatua changamoto hizo zilizojitokeza katika zoezi hilo kwa utatuzi kwa njia ya amani kwa kuzingatia haki.
Mapema mwezi Machi mwaka huu, Serikali za pande zote mbili Tanzania na Kenya zilikubaliana kuanza kazi ya uimarishaji wa mpaka wa Kimataifa katika urefu wa kilomita 238 za nchi kavu kutoka ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natroni mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment