WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula
nchini imeimarika na kufikia tani milioni 15.9 kwa msimu wa mwaka
2016/2017 na 2017/2018 sawa na kuwa na ziada ya tani milioni 2.6.
Pia
Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa
kuiwezesha Wizara ya Kilimo kuongeza uwezo wa hifadhi ya Taifa ya
chakula kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka
2025.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Aprili 21, 2018) wakati akiweka
jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa
vya kuhifadhia chakula, Kizota mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu amesema mkakati huo utahusisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata
mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa nje ya
nchi na hivyo kutoa fursa za ajira na kuwaongezea kipato wananchi.
Amesema
Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko
ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga
maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji
mkubwa wa chakula.
Pia
Waziri Mkuu amewasihi wananchi watumia fursa za kiuchumi kwenye maeneo
ambayo mradi huo utatekelezwa kwa lengo la kuboresha na kuinua hali zao
za maisha, hivyo watakuwa na uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi
wa Taifa.
Amesema
Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo mkubwa na baada ya
kukamilika utakuwa na faida kubwa kwa Taifa, hivyo amewataka viongozi wa
NFRA wahakikishe kwamba hakuna mahindi yatayoharibika katika maghala
yao.
”Mikakati
ya Serikali ni kuhakikisha NFRA inakuwa na uwezo wa kuhifadhi akiba ya
kutosha ya chakula kwa ajili ya dharula lakini pia kuweka mazingira
rafiki ya kuwezesha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao nje ya
nchi bila vikwazo”.
Hata
hivyp, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na
Mipango na Wakuu wa Mikoa ambayo mradi huo unatekelezwa na Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanatimiza wajibu wao ili mradi
ukamilike kwa wakati.
Naye
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Bibi Vumilia Zikankuba alisema mradi
huo unatekelezwa katika maeneo manane ya Kanda za Wakala huo ambayo ni
Dodoma (Dodoma), Mpanda (Katavi), Songea (Ruvuma), Makambako (Njombe),
Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga (Shinyanga), Babati
(Manyara).
Bibi
Vumilia alisema katika Kanda ya Dodoma wanajenga vihenge vyenye uwezo wa
kuhifadhi tani 20,000 na kufanya kanda hiyo kuwa na uwezo wa kuhifadhi
tani 59,000 kutoka uwezo wa sasa wa tani 39,000.
Alisema
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo
wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni
124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi
ya chakula.
“Utekelezaji
wa mikataba kati ya NFRA na wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo
muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji
wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya 2020 utakuwa umekamilika”.
Hafla
hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai , Waziri wa Kilimo Dkt.
Charles Tizeba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana,
Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama.
Wengine
ni Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi na
Ajira, Anthon Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya naBalozi wa Poland nchini Tanzania, Balozi Krzysztof Buzalski.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAMOSI, APRILI 21, 2018.
No comments:
Post a Comment