Na Ferdinand Shayo,Arusha .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo amekanusha vikali maonyesho ya Jeshi la polisi yanayoambatana na mazoezi ya jeshi hilo yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid vilivyoko jijini Arusha kuhusishwa na maandalizi ya kukabiliana na maandamano yanayohamasishwa kwenye mitandao na kudaiwa kufanyika april 26.
Mkumbo amesema kuwa maonyesho hayo ni ya kawaida na jeshi hilo limekua likijiweka imara kwa ajili ya kulinda raia na mali zao na taifa kwa ujumla na si maandamano ambayo ni ya kusadikika .
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake amesema kuwa maonyesho hayo yatafanyika April 7 baada ya kuzindua nyumba za kuishi za jeshi la polisi zitakazozinduliwa na Raisi John Pombe Magufuli.
Aidha amewakaribisha wananchi wa Jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi kuona maonyesho ya kazi za jeshi hilo lenye jukumu la kulinda raia na mali zao.
Kamanda amesema kuwa licha ya uzinduzi wa nyumba hizo wanatarajia kuzindua kituo cha utalii na diplomasia ambacho kitasaidia shughuli za utali na kuchochea ari ya watalii kutembelea mkoa wa Arusha wenye vivutio vingi.
Alisema kuwa mpaka sasa maandalizi yako vizuri ya kumpokea Raisi na wanatarajia hakutakua na msongamano wa magari kwani shughuli za kila siku zitaendelea kama kawaida.
Hata hivyo ametoa onyo kali kwa wanaoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara kwani jeshi hilo halitawavumilia na hatua kali zitachukuliwa
No comments:
Post a Comment