WAKATI kikosi cha Simba kikijiandaa kupambana na Yanga, Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, washambuliaji wa timu hiyo, Mganda, Emmanuel Okwi na John Bocco wamewashangaza wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Imebainika kuwa wachezaji hao wawili wamefanikiwa kuandika rekodi ya pekee ndani ya klabu hiyo ambayo haijawahi kuandikwa na washambuliaji wengine waliowahi kuitumikia timu hiyo kwa zaidi ya miaka sita.
Rekodi hiyo ambayo wameiweka wachezaji hao ni ya kufunga mabao mengi mpaka sasa kushinda pacha za washambuliaji wengine waliowahi kuitumikia timu hiyo katika miaka sita iliyopita.
Okwi na Bocco wameifungia Simba mabao 33 kati 58 ambayo timu hiyo imeshafunga kwenye ligi kuu msimu huu huku ikiwa na mechi tano mkononi ili kumaliza ligi hiyo.
Msimu wa 2011/12, safu ya ushambuliaji ya Simba ilikuwa ikiundwa na Okwi na Mzambia, Felix Sunzu ambapo mpaka mwisho wa msimu walifunga mbao 19 kati 47. Okwi alifunga mabao 12 huku Sunzu akifunga mabao 7.
Msimu wa 2012/13, safu ya ushambuliaji ya Simba iliundwa na Sunzu pamoja na Mrisho Ngassa ambapo ilifunga mabao tisa kati ya 38. Sunzu alifunga mabao matano huku Ngassa akifunga mabao manne.
Msimu wa 2013/14, kulikuwa na Mrundi Amissi Tambwe na Betram Mwombeki ambapo mpaka mwisho wa msimu walifunga mabao 23 kati 41 ambayo timu hiyo ilifunga. Tambwe alifunga mabao 19 na Mwombeki alifunga manne.
Msimu uliofuata wa 2014/15, Okwi pamoja na Ibrahim Ajibu walifanikiwa kufunga mabao 18 kati ya 38. Okwi alifunga mabao 10 na Ajibu alifunga mabao nane.
Katika msimu wa 2015/16, Simba ilimaliza ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 45 ambapo mabao 28 kati ya hayo yalifungwa na pacha ya timu hiyo iliyokuwa ikiundwa na Mganda, Hamis Kiiza aliyefunga mabao 19 pamoja na Ajibu aliyefunga mabao tisa.
Pacha ya mwisho ni ile ya msimu wa 2016/17 iliyokuwa ikiundwa na Shiza Kichuya na Mrundi, Laudit Mavugo ambayo ilimaliza ligi ikiwa imefunga mabao 19. Kichuya alifunga mabao 12 huku Mavugo akifunga mabao saba.
Kutokana na hali hiyo pacha ya Okwi na Bocco ndiyo pacha hatari zaidi kutokea Simba kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.
Kwa sasa wachezaji hao wanapambana kuvunja rekodi ya ligi kuu iliyowekwa na pacha ya washambuliaji wa Yanga msimu wa 2015/16 ambao ni Tambwe na Donald Ngoma waliofunga mabao 38 msimu huo. Katika msimu huo, Tambwe alifunga mabao 21 huku Ngoma akifunga 17.
No comments:
Post a Comment