Wakati Wakristo wote na wasio Wakristo duniani wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka juzi na jana, muigizaji wa sinema nchini, Elezabeth Michael ‘Lulu’ na viongozi wa Chadema walioko Gereza la Segerea jijini Dar, wametikisa viunga vya gereza hilo kutokana na uwepo wao wakati wa sikukuu.
Lulu na Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine watano wa Chadema walitikisa juzi Jumapili baada ya watu mbalimbali walipokuwa wakitaka kwenda kula nao Pasaka lakini ghafla kukasambaa ujumbe mitandaoni, uliokuwa ukieleza kuwa hairuhusiwi kuwaona mahabusu siku hizo.
“Yani huku gerezani kila mtu anajadili tu kuhusu kula sikukuu na viongozi wa Chadema na huyu muigizaji Lulu.
“Watu wamesambaziana ujumbe mitandaoni kuwa tumewazuia watu kuja huku gerezani kuja kuona jamaa zao kitu ambacho si cha kweli. Sasa wamefanya watu wengi wawajadili sana hawa huku wengi wakishindwa kuja kwa kuogopa kwamba hawataruhusiwa,” alisema askari mmoja wa magerereza aliyeomba hifadhi ya jina kwa kuwa si msemaji gazeti hili lilipotembelea gereza hilo.
Hata hivyo, ujumbe huo ulibainika kuwa haukuwa na ukweli wowote kwani baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Mbunge wa Mikumi, waliruhusiwa kwenda kuwaona.
Akizungumza na Uwazi mara baada ya kutoka gerezani humo, Profesa Jay alisema Mbowe amempa ujumbe kwamba kinachotokea sasa hivi ni harakati za ukombozi.
Alisema matendo kama ya viongozi kuwekwa mahabusu, watu kupotea, kuvunjwa miguu na kuteswa ni jambo la kawaida katika kuelekea kwenye ukombozi kama Musa alivyowakomboa wana wa Israeli.
Lulu.
Katika hatua nyingine, askari magereza aliyezungumza na Uwazi, alisema licha ya viongozi hao kuwa gumzo siku hiyo ya Pasaka, bado ndugu na jamaa waliweza kuwatembelea ndugu zao waliopo gerezani kwa makosa mbalimbali.
“Gumzo limekuwa kubwa sana kuhusu hawa kina Lulu na akina Mbowe lakini kimsingi sisi hatukuzuia watu kama walivyotumiana jumbe mitandaoni,” alisema askari huyo.
Mbali na Mbowe, viongozi wa Chadema wengine waliowekwa gerezani hapo pamoja na Mbowe ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na manaibu wake wa Bara na Zanzibar, John Mnyika na Salum Mwalimu.
Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane yakiwemo mawili ya uchochezi wa uasi yanayomkabili Mbowe.
Machi 28, mwaka huu, washtakiwa hao walifikiswa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka hayo na kukosa dhamana.
Machi 29, mwaka huu waliruhusiwa kupata dhamana mahakamani hapo lakini ikashindikana baada ya mahakama kuelezwa kuwa gari lililokuwa likiwapeleka mahabusu hao mahakamani liliharibika hivyo viongozi hao kutopelekwa mahakamani na kubaki gerezani.
Ilielezwa pia, mawakili wa upande wa serikali waliieleza mahakama kuwa wamekusudia kuweka pingamizi la dhamana hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania.
Leo, viongozi hao wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za dhamana zao.
No comments:
Post a Comment