KESI inayomkabili Tito Machibya maarufu Nabii Tito, hatma yake kujulikana Aprili 13 mwaka huu baada ya mahakama ya Wilaya ya Dodoma kupokea taarifa za kitabibu jana asubuhi.
Mahakama ya Wilaya ya Dodoma jana ilipokea taarifa ya vipimo vya kitabibu vya Tito Machibya, ilivyokuwa imeviagiza hapo awali na kumtaka afanyiwe vipimo katika Taasisi ya magonjwa ya akili ya Isanga mjini Dodoma.
Jana Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Dodoma, James Karayemaha alisema mahakamani hapo kuwa alipokea taarifa ya kitabibu kuhusu Nabii Tito kutoka Taasisi ya Isanga hivyo ataipitia na kutoa maamuzi siku hiyo ya Aprili 13.
“Nieleze kuwa nimepokea taarifa ya kitabibu kuhusu mtuhumiwa huyu leo asubuhi hivyo nitaipitia ili April 13 mwaka huu siku ya Ijumaa niweze kuitolea maamuzi,” alisema Karayemaha.
Hata hivyo Nabii Tito jana aliweza kuhudhuria mahakamani akitokea mahabusu ya gereza kuu la Isanga baada ya kutofikishwa mahakamani hapo mara mbili mfululizo.
Aidha baada ya kutofikishwa mahakamni hapo hakimu Karayemaha alimwagiza Mkuu wa gereza Isanga kuhakikisha mtuhumiwa huyo anafikishwa mahakamani hapo siku ya jana kusikiliza kesi yake inayomkabili.
Nabii Tito amerudishwa rumande hadi April 13 mwaka huu kesi yake itakapotolewa maamuzi mahakamani hapo.
Nabii Tito anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu katika mtaa huo wa Ng’ong’ona alipokwenda kukamatwa na polisi.
Baada ya kufikishwa mahakamani hapo Nabii Tito alidai kuwa yeye anamatatizo ya akili hivyo mahakama iliamuru kuwa akafanyiwe vipimo vya kitabibu katika taasisi ya magonjwa ya akili ya Isanga Dodoma.
No comments:
Post a Comment