Serikali imebariki uanzishwaji wa taasisi ya Dk. Reginald Mengi Disabled Foundation yenye lengo la kusaidia walemavu nchini.
Hilo limesemwa leo Februari 4, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hafla ya chakula cha mchana kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango wa Mengi katika uthamini wa walemavu ambapo hafla hiyo imefanyika kwa miaka 25 na itaendelea kuwa endelevu hivyo Serikali imeridhia taasisi kuanzishwa.
“Tunataka tufanye uamuzi wa kuungana na wewe, usilifanye jambo hili kama Dk Mengi pekee mimi napendekeza ulifanye kitaasisi, uunde taasisi kwa jina lako ambalo Serikali tumeridhia litumike, Reginald Mengi Disabled Foundation kwa kazi nzuri nataka jina lako liingie kwenye vitabu vya Serikali,” amesema Majaliwa.
Majaliwa ameanza kwa kuichangia Sh10 milioni ambayo itaingia pindi usajili wa taasisi hiyo utakapokamilika kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Majaliwa ameelezea hatua mbalimbali Serikali inazochukua dhidi ya walemavu ikiwa ni kila halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha, kutenga maeneo kwa ajili ya biashara na ujenzi wa majengo utakaowekwa eneo la kupandia walemavu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu) , Stella Ikupa amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakuta walemavu na inahakikisha inazitatua.
Katika hafla hiyo Mkurugenzi wa kampuni ya Kamal Group inayojihusisha na utengenezaji wa nondo walitoa msaada wa miguu bandia kwa baadhi ya walemavu wa miguu.
Mengi amesema amekuwa akifanya hafla hiyo kwa miaka 24 na itakuwa endelevu kila mwaka.
Mwananchi:
No comments:
Post a Comment