Klabu ya Simba imekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi.
Lengo ni kuwahamasisha wachezaji wake kuendelea kujituma na kusaidia matokeo bora.
Kwa mambo yalipofikia sasa, Emmanuel Okwi na John Bocco wamefanya vizuri zaidi na kusababisha kuwepo na ugumu wa kuamua, nani abebe tuzo hiyo.
Tangu ligi ilipoanza kurindima baada ya kupisha michuano ya Mapinduzi Cup, Okwi na Bocco wamekuwa wakizidi kuonyesha kiwango kizuri cha ufungaji mbapo tayari Okwi ana mabao 12 huku Bocco akiwa na mabao saba.
Chanzo kimeeleza, uongozi na benchi zima la ufundi la Simba limekuwa katika wakati mgumu wa kuamua nani atapewa tuzo hiyo ambayo wamekuwa wakiitoa kama motisha kwa wachezaji wao wanaofanya vizuri kwa mwezi husika.
“Kusema kweli mwezi Januari ni wa furaha kwetu Simba kutokana na matokeo mazuri ambayo tumekuwa tukiyapata, lakini kwa upande mwingine matokeo haya mazuri yanatupa changamoto sana hasa katika suala la kumpata mchezaji bora wa mwezi atakayepata hiyo tuzo.
“Ukiangalia vizuri kila mchezaji anajituma tofauti na huko nyuma ila changamoto kubwa inakuja kwa Okwi na Bocco ambao wote wanafanya vizuri.
"Unajua wamekuwa wakifunga kwa kufuatana, jambo ambalo tunashindwa tufanye nini kwani tumeomba hata benchi la ufundi litusaidie kumpata mtu huyo lakini wameshindwa kumchagua nani apewe tuzo hiyo jambo ambalo linatuumiza kichwa kabisa.”
Hata hivyo kwa namna hali inavyokwenda, Bocco kwa kuwa amefunga mabao matano, anaonekana ana nafasi zaidi pia ya kushinda.
No comments:
Post a Comment