Hayo yalijiri jana 12/2/2018 katika mkutano wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ndg.John L.Kayombo katika ukumbi wa Manispaa Kibamba ambapo umehudhuriwa na Wenyeviti wa mitaa ,wajumbe wa serikali za mitaa , wataalamu wa Manispaa na wale wanaojiita Wamiliki wa vibanda vya Maduka na wapangaji wa fremu za mtaa wa Tupendane na Muungano kata ya Manzese.
Akiongea mara baada ya kufungua mkutano huo Mkurugenzi alisema ameitisha mkutano huo kwa lengo la kuja kuwaambia wazi msimamo na maamuzi ya serikali juu ya maeneo ambayo ni mali ya serikali.
Wakitoa maelezo mbalimbali waliyotakiwa kuyatoa na Mkurugenzi kuhusu umiliki na ulipaji wa kodi ,wapangaji walielezea jinsi ambavyo wamekuwa wakilipa kodi kwa wanaowapangisha ambapo baadhi wamekuwa wakiingia mikataba ya kupangisha na kulipa kodi kwa mwezi 200000/=, 300000/=,hadi 350000/= ambapo manispaa imekuwa hainufaiki na pesa hizo na kupoteza mapato ya serikali aidha wanaojiita wamiliki walipoulizwa kuhusu hati za umiliki hawakuweza kuonyesha hati hizo zaidi ya kueleza kuwa waliandika barua za maombi ya kumiliki maeneo hayo kupitia kwa wenyeviti kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.
Wajumbe pia wametoa malalamiko yao kuwa wamekuwa hawashirikishwi na wenyeviti wao katika maswala hayo na hawajui chochote kinachoendelea zaidi ya kupewa taarifa zisizo sahihi na wenyeviti wao kuhusu maeneo hayo na fremu hizo katika mitaa hiyo.
Akiongea baada ya kusikiliza kwa muda maelezo mbalimbali kutoka kwa Wenyeviti,wapangaji,wajumbe na wamiliki Mkurugenzi Kayombo alitoa maamuzi mazito 4 kama ifuatavyo:
a) Mikataba yote iliyoingiwa kati ya walaghai na wapangishaji wa fremu hizo ni feki na kuanzia leo(12/2/2018)haitambuliki na manispaa na imefutwa
b) Maeneo na fremu hizo kuanzia sasa yanarudishwa na kurejeshwa rasmi serikalini kama ambavyo inaonyesha katika ramani kuwa ni maeneo ya umma*
C)Wale wote waliokuwa wakijiita ni wamiliki kuanzia sasa ni wapangaji wa Manispaa na tutatoa utaratibu mpya wa kiwango cha kulipia moja kwa moja kwenye akaunti za Serikali.
D)Wapangaji wote katika fremu hizo watapewa utaratibu na manispaa baada ya mkutano huu kwani kuanzia leo na wao ni wapangaji wa Manispaa.
Jumla ya vibanda vya maduka 30 vimerejeshwa Serikalini ambavyo vilikuwa vinamilikiwa na wananchi kinyume na utaratibu kuanzia mwaka 1997 kwa Mtaa wa Muungano na Pia mwaka 2000 kwa mtaa wa Tupendane Zenye mikataba ya zaidi ya miaka 35
Akiongezea mara baada ya kutoa maamuzi hayo amesema asitokee mtu yoyote kuwatishia wala kuwapa usumbufu wapangaji hao na manispaa ipo pamoja nao. Aidha amesema itasainiwa mikataba mipya ( kati ya Manispaa na waliokuwa wapangaji , wamiliki) ambao sasa ni wapangaji wa manispaa kwani mwenye uhalali wa kusaini mikataba katika maeneo ya umma ni Meya na Mkurugenzi na si vinginevyo
Katika hatua nyingine Mkurugenzi amewataka wenyeviti kuacha kuingilia majukumu yasiyowahusu wafanye majukumu ambayo ni haki yao kwani wamekuwa awakiingilia majukumu ya watendaji na wahasibu ambao wanamuwakilisha Mkurugenzi katika kata husika.
Amewakumbusha pia kuwa serikali hii ipo makini katika kuhakikisha mali za umma zinawanufaisha wananchi wote na si kuibiwa watu wachache na kuwanufaisha kundi la watu flani.
"Huu ni muendelezo wa kuhakikisha tunarudisha maeneo yote ya umma yanayotumika kunufaisha wavamizi tumeanzia Kata ya Sinza kwa kuweka alama ya X maeneo yaliyovamiwa na sasa tumekagua hapa manzese na tutaendelea katika kata zingine zote,siwezi kufumbia macho uvamizi wa maeneo na watu kujinufaisha kupitia maeneo hayo ya umma
Nae Mwenyekiti wa wenyeviti kata ya manzese alimshukuru mkurugenzi kwa niaba ya wenzake kwa busara zake katika kushughulikia jambo hili na kumpongeza kwa kasi yake ya uchapaji kazi kama ambavyo serikali ya awamu ya tank imekuwa ikitaka na kuendana na kasi ya Mh. Rais Dkt.John Pombe Magufuli.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO MANISPAA YA UBUNGO
No comments:
Post a Comment