A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Monday, February 26, 2018

Kakobe ainyambua taarifa ya TRA

Siku sita baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa taarifa ya uchunguzi katika Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Zachary Kakobe ameibuka na kuipangua huku akiishangaa taasisi hiyo ilivyoanika barua yake ya siri aliyomwandikia Rais John Magufuli.

Akizungumza jana katika kanisa hilo lililopo Mwenge, jijini Dar es Salaam, Askofu Kakobe aliyekuwa akishangiliwa mara kwa mara na waumini wake alianza moja kwa moja kujibu taarifa hiyo ya TRA mara tu baada ya kupanda madhabahuni kuanzia saa 7:14 mchana hadi saa 10:7 jioni, “Yapo mambo kadhaa yaliyopotoshwa ambayo yanatakiwa kunyooshwa,” alianza.

“Swali linakuja, kwa nini watu hawa miaka yote walikaa kimya leo wanaibuka na kusema kanisa langu linakwepa kodi? Taarifa hii ni ya kishilawadu, kisiasa na inayolenga kunichonganisha na waumini wangu.”

Shilawadu ni kipindi kinachorushwa na televisheni ya Clouds kila siku ya Ijumaa, kikizungumzia zaidi maisha binafsi ya wanamuziki, wasanii na watu maarufu.

TRA ilifanya uchunguzi huo kutokana na kauli ya Askofu Kakobe aliyoitoa alipozungumza na waumini wake katika mkesha wa Krisimasi mwishoni mwa mwaka jana kwamba ana fedha kuliko Serikali.

Baada ya kauli hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema watafanya uchunguzi kubaini utajiri huo.

Baadhi ya mambo ambayo Kichere alieleza TRA kuyabaini baada ya uchunguzi huo ni; Askofu Kakobe kutokuwa na akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya fedha nchini zaidi ya kuwa mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti ya kanisa, akaunti za kanisa zipo katika Benki ya NBC zikiwa na zaidi ya Sh8 bilioni.

Nyingine ni kanisa hilo kukwepa kodi ya Sh20 milioni, kampuni inayomilikiwa na watoto wa Askofu Kakobe ilikwepa kulipa kodi ya Sh37 milioni ambazo zote zimelipwa baada ya uchunguzi.

Nyingine ni kanisa hilo kutunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na majaba kinyume cha utaratibu wa utunzaji fedha, uwekaji na utoaji wa fedha nyingi benki bila ya kushirikisha vyombo vya ulinzi pamoja na fedha za kanisa kutumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu Kakobe kwa jila lake badala ya kanisa, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa kanisa.

Pia, Kichere alieleza kuwa Askofu Kakobe alimuandikia barua Rais Magufuli kuomba radhi kutokana na kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya dharau kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali.

Majibu ya Kakobe

Huku akizungumza kwa makini, Askofu Kakobe alianza kwa kuzungumzia barua iliyoelezwa na TRA kwamba alimuomba radhi Rais, “Kwanza nashangaa, mimi niliandika waraka wa kichungaji wa siri kwa Rais juu ya mambo kadha wa kadha nikimpongeza kwa kazi yake na niliandika kwa heshima iliyotukuka.”

Alisema barua hiyo aliandika bila kuwashirikisha wasaidizi na waumizi wake, kwamba kitendo cha TRA kuiweka wazi kimemsikitisha kwa sababu mamlaka hiyo si msemaji wa Rais.

“Siwezi kuomba radhi wala msamaha kwa mtu wa aina yeyote. Nilichokiandika katika waraka kwa Rais ni sauti ya Mungu, kama wanataka wamwambie Mungu aombe msamaha si Kakobe. Mungu ndiye aliyezungumza.”

Kuhusu uchunguzi wa TRA, alisema baada ya taarifa hiyo kutolewa aliamua kukaa kimya licha ya watu kumtaka ajibu kwa sababu katika kipindi hicho kulikuwa na mambo muhimu ya kitaifa yaliyokuwa yakijadiliwa.

“Ningejibu wakati ule majibu yangu yangekuwa habari kubwa, kwa sasa ninaweza kuzungumzia taarifa ya TRA,” alisema Kakobe huku akiuchambua uchunguzi huo wa TRA.

“Kamishna wa TRA alishukuru namna nilivyompa ushirikiano mzuri juu ya uchunguzi wao. Walitumia nguvu kubwa kuchunguza na walithibitisha kuwa sina fedha katika taasisi yoyote ile. Sina mradi, sina shamba wala sifugi hata panya.”

Alisema katika uchunguzi huo, TRA walibaini kuwa mke wake hana mradi wala fedha zozote kwenye taasisi na kwamba aliwaeleza fedha alizonazo zinatokana na wito wake kama walivyo watu wengine.

“Katika taarifa yao kuna mambo mengi yaliyopotoshwa, sina uhakika kama ni kwa makusudi. Mnakumbuka Januari 14 siku ya Jumapili kama leo (jana) niliwaeleza kuwa kuna njama na hila zinazopangwa juu ya kupotosha ukweli wa mambo,” alisema.

Alisema TRA walikwenda nyumbani kwake na kanisani kufanya upekuzi hadi chumbani kwake, “Nikawaeleza atakayeona kitu chochote kinachoashiria mimi ninakwepa kodi basi nitampa zawadi.”

Alisema maofisa wa TRA pia walibaini kuwa kanisa lake ni safi na halina shida yoyote na kusema alishangaa jambo hilo kutoandikwa katika taarifa ya mamlaka hiyo.

“Walishangaa ninaishi katika nyumba ambayo haifanani na hadhi yangu na heshima kubwa niliyonayo. Walisema sifai kuishi katika nyumba hiyo kwani si ya kiwango changu,” alisema.

Alisema kutokana na hilo, maofisa hao walitoa ushauri kwa washirika wa kanisa lake, kwamba mpango walionao wa kumjengea nyumba ufanyike haraka ili aweze kutoka katika nyumba anayoishi sasa.

“Waliyozungumza kwenye taarifa yao yanachanganya. Mfano, wamesema kanisa hili lina akaunti kwenye benki ya biashara (NBC) na kutaja kiasi cha fedha katika akaunti wakati ni kinyume na sheria za kibenki,” alisema.

Alisema akaunti hiyo ipo tangu miaka ya 1990 na kwamba taarifa ya TRA imemsikitisha yeye na waumini wake na kumfanya aamini kuwa uchunguzi dhidi yake umefanyika kisiasa, si kisheria.

“Wamesema tuna akaunti benki ya biashara, wakasema na kiasi kilichopo lakini wakati huohuo wanasema tuna fedha tumehifadhi kwenye ndoo na majaba,” alisema na baadhi ya waumini kuitikia, “Ni siasa hizo.”

“TRA wamesema fedha zilizoko benki zina wasimamizi sita ma-signatory (watia saini) mimi nikiwa msimamizi mkuu wa fedha hizo. Sasa najiuliza mimi ni msimamizi wa fedha za benki au za kwenye ndoo na majaba.”

Wakati Kakobe akieleza kuhusu ndoo na majaba, waumini walikuwa wakinyoosha juu ndoo na majaba hayo.

“Sasa wanataka sadaka zikusanywe kwenye khanga na vitenge? Kazi ya ndoo hizi ni kukusanya fedha zinazotolewa na waumini kanisani kama ilivyo makanisa mengine na baada ya hapo fedha hizo hukusanywa na kupelekwa benki,” alisema.

Alidai kwamba alishaonyeshwa na Mungu kwamba uchunguzi huo wa TRA dhidi yake lengo lake ni kumchonganisha na waumini wake, kuwataka wazipuuze.

“Kunichonganisha mimi na nyinyi hiyo ni biashara ya kichaa. Majaribio haya yamefanyika kwa zaidi ya miaka 10 lakini hawakufanikiwa,” alisema Kakobe.

Alisema waumini wake wanamuamini kuliko wanavyowaamini wazazi wao na kwa heshima huwa wanamuita baba na wanaogopa kumuita Kakobe.

“Ni rahisi kuwachonganisha waumini wangu na wake zao au waume zao lakini si kuwachonganisha na baba yao (Kakobe).Wangapi wananiamini,” alihoji na kujibiwa na waumini hao huku wakinyoosha mikono juu na kupiga makofi.

Kuhusu kusafiri na mkewe nje ya nchi, Askofu Kakobe alisema, “TRA wanalalamika kuwa natumia fedha vibaya kwenda nje na familia yangu. Hili jambo si kweli.”

Aliwaita madhabahuni waumini wake waliowahi kusafiri nje ya nchi kwa fedha za kanisa na kuwapa kipaza sauti na kutaja nchi walizowahi kwenda.

“Sasa hawataki nisafiri na mke wangu kwenda nje ya nchi wanataka nisafiri na changudoa? Hawajui kuwa mke wangu ndio mlinzi, hata changudoa akigonga mlango mke wangu ataamka na kwenda kumfungulia,” alisema.

Kuhusu fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye kampuni iliyowahusisha watoto wake, alisema zilikuwa fedha ambazo waumini wake walichangisha kwa ajili ya kumjengea nyumba na ziliwekwa katika akaunti nyingine ili wapate riba.

“Zilivyofikia malengo, zilitolewa na kuingizwa katika akaunti ya kanisa. TRA walisema zilitolewa bila kufuata utaratibu na hazijalipiwa kodi. Tuliamua kuzilipa hizo fedha,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages