Wanakikundi
cha Upendo kilichopo Kijiji cha Magiri Kata ya Magiri katika Halmshauri
ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakiwa pamoja na watafiti kutoka Tume
ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Jukwaa la Bioteknolojia kwa
Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku
mkoani Kagera na Mwanahabari Coleta Makulwa wa RFA (wa pili kushoto),
baada ya kukabidhiwa mbegu bora za Viazi lishe aina ya Kabode kwa ajili
ya kuzipanda kwenye shamba darasa katika kata hiyo wilayani humo leo.
Mbegu hizo zikiinuliwa juu baada ya kukabidhiwa.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akimkabidhi mbegu za mihogo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Uyui, Hadija Makuwani kwa ajili ya
kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Isikizya wilayani humo.
Wengine ni wakulima wa kijiji hicho.
Wanakikundi cha Mapambano katika Kijiji cha Iberamilundi wakifurahi mbegu bora ya mihogo baada ya kukabidhiwa.
Wakulima wa Kijiji cha Isikizya wakiwa kwenye uzinduzi wa shamba darasa.
Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH,
Audax Mutagwa, akizungumza na wakulima na wakulima wa Kijiji cha
Isikizya (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Mshauri wa Jukwaa la
Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange na
Mtafiti kutoka COSTECH, Bestina Daniel.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Wilaya ya Uyui, Hadija Makuwani akizungumza na wakulima
kabla ya kuzindua shamba darasa la mbegu ya mihogo katika Kijiji cha
Isikizya.
Wakulima wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Mkulima, Gervas Fungameza akiuliza swali.
Mkulima Said Mirambo wa Kijiji cha Isikizya akiuliza swali.
Mtafiti
wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku
mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akielekeza ubora wa mbegu ya mihogo aina
ya mkombozi jinsi ya kuipanda
Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Hadija Makuwani akizindua shamba darasa hilo kwa kupanda mbegu ya mihogo.
Diwani wa Kata ya Isikizya akipanda mbegu hiyo.
Kaimu
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Uyui, Hamphrey Kilua akizungumza na
wanakikundi cha Mapambano kabla ya kuzindua shamba la Viazi lishe katika
Kijiji cha Iberamilundi.
Wanakikundi cha Iberamilundi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Mtafiti
wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku
mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wanakikundi cha Mapambano
cha Kijiji cha Iberamilundi namna ya kupanda mbegu ya mihogo katika
shamba darasa.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Jumanne Said Mnubi
akipanda mbegu hiyo.
Katibu wa Kikundi hicho, Clementina Nyamizi akipanda
mbegu katika shamba darasa.
Wanakikundi cha Upendo cha Kata ya Magiri wakiwa na mbegu zao mkononi za Viazi lishe
Na Dotto Mwaibale, Uyui Tabora
HALMASHAURI
ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora imezipokea kwa mikono miwili mbegu bora
za mahindi aina ya Wema, Viazi lishe na mihogo zilizotolewa na Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la
Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)
Mbegu
hizo zimetolewa katika vijiji vitano vya wilaya hiyo kwa ajili ya
kuanzisha mashamba darasa ambavyo vimetajwa kuwa ni kijiji cha Isikizya
kilichopo Kata ya Isikizya ambacho kitakuwa na shamba darasa la zao la
mihogo, Ibelamilundi ambacho pia zao lake ni mihogo, Kijiji cha Kigwa
ambacho zao lake ni Viazi lishe, Igalula ambacho kitapandwa mahindi na
Magiri ambacho kitakuwa na shamba darasa la zao la Viazi lishe.
Akizungumza
wakati wa kupokea mbegu hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Hadija
Makuwani alisema wao kama wilaya wamezipokea mbegu hizo kwa mikono
miwili na watazifanyia kazi ili waweze kupata mazao yenye tija.
"Kwa
kweli tunawashukuru sana COSTECH na OFAB kwa kutuletea mbegu hizi kwani
tuna imani zitatuondelea changamoto ya kupata mazao machache kutokana
na kutumia mbegu za kienyeji zilizozoeleka kwa wakulima wetu" alisema
Makuwani.
Makuwani
alisema hata yeye kwa kuwa ni mkulima anaomba apatiwe mbegu hizo ili
akazipande kwenye shamba lake ili hapo baadaye nawe aweze kusambaza
mbegu hiyo.
Diwani
wa Kata ya Isikizya, Ally Mtelela alisema mbegu hizo zitazidisha ari
kwa wakulima hao na wataondokana na kilimo kisicho na tija ambacho
walikuwa wakitumia mbegu ambazo zilikuwa zikishambuliwa na magonjwa.
Mtafiti
wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha ARI-Maruku
mkoani Kagera, Jojianas Kibura aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja
ya mihogo iwapo watalipa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza
kupata tani 25 hadi 32 na kwa zao la viazilishe watapata tani 7 hadi 9
kwa hekta moja.
Alisema
matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha
mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa
mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi
tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane
hadi kumi wakati kwenye Viazi lishe wanapata tani moja hadi tatu.
Kibura
alisema Viazi lishe hivyo aina ya kabode vina vitamini A ambavyo ni
muhimu kwa watoto kwa lishe na rangi yake ni vya njano na vinaisaidia
serikali kuacha kutumia matone ya vitamini A badala yake mtu akivila
anapata vitamini hiyo moja kwa moja.
Akizungumzia
kuhusu mbegu Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa
Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hizo ya mihogo aina
ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana ina uwezo mkubwa wa
kustahimili magonjwa kama ya batobato kali na michirizi ya kahawia
ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima na ya mahindi
ikistahimili hali ya ukame na kutoa mazao mengi.
Mutagwa
aliwaomba wakulima hao kuyatunza mashamba hayo ambayo yamegharimu fedha
nyingi hadi kukamilika kwake hivyo wayaendeleze kwa ajili ya kuja kutoa
matunda kwa wakulima wa wilaya hiyo na kupata chakula cha kutosha na
ziada kuuza.
Mkulima
Clementina Nyamizi wa Kijiji cha Iberamilundi ambaye ni Katibu wa
Kikundi cha Mapambano alisema wanaamini mbegu hizo zitawatoa katika
umasikini na kuwa watazitunza na kuzilinda na wataachana kabisa na mbegu
za kienyeji walizokuwa wakizitumia zamani.
No comments:
Post a Comment