Na. Prisca Libaga-MAELEZO, Arusha.
Mamlaka
ya chakula na dawa TFDA imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu
magonjwa ya binadamu na kuziondoa kwenye soko pamoja na kusitisha
matumizi yake kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.
Hayo
yameelezwa jana Jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti
Sillo, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya wakufunzi wa
ufuatiliaji juu ya ufundishaji na uhamasishaji wa masuala ya udhibiti wa
madhara yatonayo na matumizi ya dawa zisizosalama kwa watendaji wa afya
kutoka Wilaya zote za mkoa wa Arusha.
Bw.
Sillo mesema katika kudhibiti matumizi ya dawa zisizofaa TFDA imeondoa
dawa ya sindano aina ya Chloramphenical kwenye soko baada ya shirika la
afya Duniani WHO, kubaini dawa hiyo ina madhara kwa watumiaji, Pia
mamlaka hiyo imefuta usajili wa dawa zingine kama vile Ketoconazole,
(vidonge) Phenylpropanalamine,Dextropropoxyphene,Nimesulide,stavudine
40, Gatifloxacin,Rofecoxib, pamoja na Celecoxib baada ya kuthibitika
zina madhara kwa watumiaji.
Aidha
matumizi ya dawa kama vile Kanamycin,Amikacin na Levofloxacin
zimebadilishwa ili ziweze kutumika kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa kifua
kikuu pekee.
Mkurugenzi
huyo wa TFDA amesema mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini
kote na yanafanyika katika mikoa mbalimbali yakiwashirikisha Madaktari,
Manesi, na wafamasia walioko kwenye hospitali, vituo vya afya na
Zahanati.
Bw.Sillo
alieleza kwamba, lengo la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi
wa masuala ya usalama wa dawa kutoka 73 hadi 133 na tayari katika
kipindi cha miaka mitatu 2014/ 15 hadi 2017/18, Mamlaka ya chakula na
dawa imehamasisha watendaji wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa
uhamasishaji unaendelea katika mkoa wa Katavi.
Alisema
mara baada ya mafunzo hayo wakufunzi hao watafundisha wenzao kwenye
maeneo yao ya kazi ili kuongeza uelewa kwa wataalam wengi zaidi kufahamu
taratibu zilizoko za udhibiti wa madhara yanayotokana na matumizi ya
dawa zisizofaa.
Aliwakumbusha
wakufunzi hao kwamba kila mtendaji wa afya ana wajibu wa kulinda afya
za wagonjwa anao watibu au kuwahudumia na wajibu huo ni pamoja na
kuhakikisha wagonjwa wanabaki salama na ikiwa watapata madhara hatua za
kuwatibu zinachukuliwa na kutoa taarifa ili kuzuia kusambazwa zaidi kwa
dawa zinazoleta madhara.
Bw.
Sillo alifafanua kuwa, kumekuwa na baadhi ya wataalam wa afya kudhani
kuwa kwa kutoa taarifa kuwa dawa ina madhara inaonekana kuwa wao ndio
wanaosababisha madhara hayo na kusisitiza kuwa dhana hiyo sio ya kweli,
hivyo akawasisitiza watoe taarifa sahihi ili wananchi wafahamu madhara
yatokanayo na matumizi ya dawa pamoja na hatua za kuchukua.
Mamlaka
ya chakula na dawa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma
wametengeneza mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa taarifa za usalama na
madhara ya dawa ambao ulizinduliwa Oktoba 2016 na Waziri wa afya Mh.Ummy
Mwalimu.
Kabla
ya kuzinduliwa mfumo huo taarifa za usalama na madhara ya dawa zilikuwa
zikitolewa kwa kutumia fomu maalumu za njano ,kijani na blue ambapo
watoa huduma za afya walikuwa wakitumia fomu za njano huku wagonjwa
wakitoa taarifa kwa kutumia fomu za za kijani, na fomu za bluu
zilitumika kutoa taarifa za ubora wa dawa na kama kuna dawa duni au
bandia kwenye soko.
No comments:
Post a Comment