Waziri
Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akijibu maswali mbalimbali ya wabunge wakati
wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati wa kikao cha tatu cha
mkutano wa tisa wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini
Dodoma.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza kwamba vyombo vya dola vya ndani ya
nchi havijashindwa kuchunguza matukio ya kihalifu yaliyotokea nchini,
hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa na subira.
Amesema
Serikali hairidhishwi na matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyofanywa na
watu wasiolitakia mema Taifa, ambayo yaliyotokea katika maeneo
mbalimbali nchini na baadhi yake yamesababisha vifo na wengine
kujeruhiwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 9, 2017) wakati akijibu
swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe katika kipindi
cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.
Bw.
Mbowe alitaka apew kauli ya Serikali juu ya hatua zilizochukuliwa
kuhusu tukio la kushambuliwa na mbunge wa Singida Mashariki Bw. Tundu
Lissu, ambapo alishauri uchunguzi huo ufanywe na vyombo vya kimataifa,
ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya
ndani vya dola.
“Vyombo
vya ndani vya dola vina uwezo mkubwa wa kusimamia usalama wa nchi na
vinaendelea na uchunguzi wa matukio hayo yaliyofanywa na watu
wasiolitakia mema Taifa letu. Nawaomba wananchi waendelee kuwa na imani
na vyombo vyetu vya dola na mara uchunguzi utakapokamilika taarifa
itatolewa.”
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi waendelee kushirikiana na
Serikali kwa kutoa taarifa mbalimbali juu ya vitendo vya kihalifu
vinavyotokea kwenye maeneo yao kwa lengo la kudumisha amani na utulivu
nchini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kuboresha maslahi ya watumishi wa umma imeanza kutekelezwa kwa
kuwapandisha madaraja watumishi wanaostahili sambamba na kulipa
malimbikizo yao mbalimbali.
Waziri
Mkuu amesema baada ya kumaliza ulipaji wa malimbikizo ndipo Serikali
itaendelea na hatua ya uboreshaji wa mishahara kwa watumishi wote wa
umma, hivyo amewaomba waendelee kuwa na subira na imani na Serikali.
Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilindi,
Bw. Omary Kigua aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itapandisha
mishahara ya watumishi wa umma.
Pia
Waziri Mkuu amezungumzia changamoto ya masoko kwa mazao ya mbaazi na
tumbaku ambayo yanashughulikiwa na Serikali na tayari baadhi ya nchi
zimeanza kuonyesha nia ya kununua mazao hayo, hivyo amewaomba wananchi
waendelee kuwa na uvumilivu.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu
Bibi Munde Tambwe aliyeiomba Serikali kumpatia ufafanuzi juu ya
kukosekana kwa soko la tumbaku ambayo imelundikana katika maghala na
Bibi Pauline Gekul Mbunge wa Babati aliyelalamikia kukosekana kwa soko
la zao la mbaazi.
Akizungumzia
kuhusu zao la tumbaku, Waziri Mkuu amesema changamoto hiyo imetokana na
wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji tofauti na makubaliano
yaliyofikiwa awali na wanunuzi. “Nawaomba wakulima waendelee kuwa
wavumilivu Serikali inafanya mazungumzo na nchi za lran, Korea Kusini,
Misri na Indonesia ili waweze kununua tumbaku hiyo na kuwaondolea
usumbufu wakulima.”
No comments:
Post a Comment