TIMU ya soka ya Argexas juzi
imeibuka bingwa wa mashindano ya kombe la Segerea 2017 baada ya kuichapa timu
ya Kinyerezi Fc mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika katika uwanja ya Toto Tundu
uliopo Tabata Segerea jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa
na Mbunge wa Viti maalum katika Halmashauri ya Ilala kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Anatropia Theonest yalishirikisha timu 24
za vijana.
Katika mchezo huo wa fainali
uliochezwa huku mvua kubwa ikinyesha, timu ya Argexas ilionekana kutawala
mchezo katika kipindi chote cha kwanza huku ikikosa magoli mengi ya wazi.
Hata hivyo katika dakika ya 46
ya kipindi cha kwanza kupitia kwa mchezaji Rashid Ismail, timu ya Argexas
iliweza kupata bao lake la kwanza kabla ya dakika ya pili baadae kupitia kwa
Patrick Muhagama aliyepiga shuti kali lililomfanya kipa wa Kinyerezi abaki
ameshika kichwa asiamini macho yake.
Baada ya mpambano huo
kumalizika, mshindi wa kwanza alikabidhiwa zawadi ya Ngombe, kikombe, jezi
pamoja na mpira mmoja huku mshindi wa pili ambaye ni Kinyerezi Fc alipata Mbuzi
wawili, jezi pamoja na mpira mmoja.
Timu ya Tabata Future ambayo
ilishika nafasi ya tatu ilipata jezi pamoja na mpira mmoja huku mfungaji bora
wa mashindano kutoka katika timu ya Argexas Rashid Ismaili alizawadiwa na
muandaaji wa mashindano pesa tasilimu sh 100,000.
Akizungumza baada ya kukabidhi
zawadi, Anatropia alisema mashindano hayo yatakuwa endelevu na kwamba lengo ni
kuwaweka karibu vijana pamoja na kuendesha kamapeni ya vunja ukimywa yenye
lengo la kuondoa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto katika manispaa ya
Ilala.
Alisema mashindano hayo
yalianza kutimua vumbi miezi miwili iliyopita na kwamba timu 24 zilishiriki
ambapo baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika zilibaki timu 16 ambazo kati ya
hizo nane zilifika hatua ya robo fainali na baadae nne zikacheza hatua ya nusu
fainali iliyowezesha kufikia fainali kwa kuzikutanisha timu za Kinyerezi Fc na
Argexas.
Mbunge wa Viti maalum katika Halmashauri ya Ilala kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Anatropia Theonest akimkabidhi zawadi mfungaji bora kutoka katika
timu ya Argexas ambayo ndio bingwa wa mashindano alimzawadia pesa taslimu sh
100,000.
No comments:
Post a Comment