Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri ameagiza kuanzia msimu ujao wa
kilimo kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi ni lazima alime heka mbili
za alizeti kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kujenga Viwanda vya kusindika
na kuzalisha mafuta hayo kuanza ujenzi mkoani humo.
Bw. Mwanri
alitoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi wa maonesho ya nanenane kwa
Kanda ya mikoa ya Magharibi yaliyofanyika mkoani Tabora.
Alisema
zao la alizeti katika mkoani Tabora linastawi sana na ikiwa wakazi wake
watalima kwa wingi Kampuni mbalimbali zitajitokeza kwa wingi kuja
kujenga viwanda vya kuzalisha mafuta hayo.
Bw.Mwanri alisisitiza
kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wanashindwa kuja kujenga viwanda vya
usindikaji wa mafuta hayo kwa sababu siku za nyuma zao hilo limekuwa
halitiliwi mkazo na kufanya uzalishaji kuwa wa chini sana , lakini hivi
sasa hiyo itakuwa ajenda ya Mkoa kama mkakati mojawapo wa kuwavutia watu
kuja kujenga viwanda.
“Ndugu zangu Wakuu wote wa Wilaya na
Wakurugenzi kuanzia sasa akili yetu na agenda yetu kubwa iko katika
kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Tabora analima heka mbili za alizeti
kuanzia msimu ujao wa kilimo ili tuwe na malighafi nyingi kwa ajili ya
kulisha viwanda vitakavyoanzishwa kwa mwaka mzima” alisema Mkuu huyo
Mkoa.
Katika kutekeleza agizo hilo aliwaagiza Maafisa Ugani wote
mkoani hapa kuhakikisha wanawatembelea wakulima vijijini kwa ajili ya
kuwaelimisha juu ulimaji bora na mbegu bora za zao hilo kwa ajili
kuwafanya wakulima kuanza mara moja kilimo hicho pindi mvua za masika
zitakapoanza.
Katika hatua nyingine aliwaagiza Wakurugenzi
Watendaji wote na Maofisa Ugani wote kuhakikisha kuwa wanaanza
wanawahimiza wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kuanza kilimo cha
zao la uwele , mtama, viazi na mihogo ili kukabiliana na tatizo la
upungufu wa chakula kwa sababu ya mvua kuendelea kunyesha chini ya
kiwango.
Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuendelea
kung’ang’ania mazao yanatumia miezi mingi kukomaa kusababisha wakazi hao
kuendelea kukabiliwa na upungufu wa chakula wakati wakilima mazao
yanayostahimili ukame tatizo haliwezi kuwapata.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Nzega alisema kuwa wao tayari wameshaanza maandalizi kwa kuwa
na shamba la mfano la heka 10 ambapo tayari wameshazalisha alizeti na
kutoa mafuta.
Alisema kinachofuata ni kuongeza wigo wa kilimo
hicho wa kuwashirikisha wananachi wengi kwa kuwaelimisha juu ya kilimo
bora cha zao hilo ili waweze kuzalisha kwa wingi na kutoa fursa kwa
wamiliki wa viwanda kupata malighafi ya kutoa kwa ajili ya uzalishaji
mafuta.
Naye Mkazi wa Ipuli mkoani Tabora Juma Elia aliunga mkono
agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora la kuhamasisha wakulima kuanza kulima
alizeti ambalo ni rafiki na mazingira kwa sababu halihitaji kuni kukauka
kama ilivyo tumbaku.
Aliongeza kuwa zao hilo litasaidia kutoa
ajira kwa njia ya vijana kushiriki kilimo na wengine kuajiriwa katika
viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti vitakavyoanzishwa.
No comments:
Post a Comment