Baada
ya kufanikiwa kulipa faini ya milioni 200 hatimae leo mfanyabiashara ,
Ndama Shabani Hussein, maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng'ombe
amepata dhamana.
Ndama
amepata dhamana baada ya kuwa na wadhamink wawili na kuwasilisha hati
ya mali isiyohamishika yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 600.
Wiki
iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimtia hatiani Ndama na
kumuhukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya milioni 200 baada
ya kukiri shtaka la kutakatisha USD 540,000.
Aidha
mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ilimsomea
masharti ya dhamana mshtakiwa huyo iwapo angefanikiwa kulipa kiasi
hicho cha milioni 200 ili awe huru katika mashtaka matano yanayoendelea
kumkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.
Katika
masharti hayo, Ndama alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na
atoe fedha taslimu kiasi cha USD 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya
milioni 600 mahakamani hapo ama mali isiyohamishika yenye thamani ya
kiasi hicho cha fedha
Licha ya kupata dhamana, Ndama amerudishwa gerezani kukamilisha taratibu kabla ya kuachiwa huru.
Hukumu
hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili
wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na
kuyakubali maelezo ya awali na maelezo yote yanayounda shtaka hilo la
kutakatisha fedha, akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.
Kabla
ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia mahakama kuwa
mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo
yanayounda shtaka hilo, hawana kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya
Ndama ila ni rai ya upande wa mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa
adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 13(a) cha sheria ya kuzuia
utakatishaji fedha.
Pia
mahakama ibebe dhana ya sheria hiyo ambayo lengo lake ni kuzuia makosa
ambayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa kosa ambalo
mshtakiwa amelifanya.
Kwa
upande wa Wakili Wabeya Kung’e anayemtetea mshtakiwa huyo kwa
kushirikiana na Jeremiah Mtobesya, Kung’e aliiambia mahakama kuwa ni
wazi mshtakiwa amekiri kosa baadaya kusomewa maelezo ya awali ni rai
yetu mahakama isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa .
Aliiomba
mahakama izingatie maombi yao kwa sababu mshtakiwa huyo hilo ndiyo kosa
lake la kwanza, kitendo chake cha kukiri kosa kinaonesha kusikitikia
kosa alilolitenda na kwamba anayo familia ambayo inamtegemea ambao kwa
kipindi cha mwaka mmoja ambacho amekaa ndani imepata shida kwa kukosa
huduma yake.
“Kwa
kuzingatia kifungu cha 13(a) cha sheria ya kutakatisha fedha ni rai
yetu mahakama tukufu isitoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwa sababu
amejutia kosa alilolitenda”Alisisitiza kueleza Kung’e. Hivyo amehukumiwa
kulipa faini ya Sh 200 milioni ama akishindwa kutumikia kifungo cha
miaka mitano jela.
Juni
6,2017 Ndama aliiomba mahakama akumbushwe shtaka, akakumbushwa na
Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na akalikubali shtaka hilo.
Akisomewa
maelezo ya awali mahakamani hapo, Ndama alikubali maelezo ya awali
aliyosomewa ikiwamo nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika
kuingizwa hizo fedha, hundi 18 zilizotumika kutolea hizo fedha, maelezo
ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.
Amekubali
kuwa Mei 14,2013 wakurugenzi ambao pia ni wanahisa wa kampuni ya Muru
Platnum Tanzania Investment Company Limited wanaotambulika Brela,
Bushoboka Mutamura na Mujibu Hamis Taratibu waliisajili kampuni hiyo
Brela na kupata hati ya usajili namba 99249 kwa ajili ya kushughulikia
biashara ya madini.
Aliendelea
kukubali kuwa Septemba 16,2013 alifungua akaunti benki ya Stanbic
katika tawi la Viwandani kwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwamo TIN
namba ya kampuni hiyo, leseni ya biashara na hati yake ya kusafiria
nakwamba wakati akiifungua alijitambulisha kuwa yeye ndiyo Mwenyekiti wa
kampuni hiyo na mtia saini pekee.
Pia
alikubali kuwa kampuni ya kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment
Company Limited iliingia mkataba na kampuni ya Trade TJL DTYL Limited ya
Australia na kwamba aliwagaia wabia wenzake fedha hizo taslimu kwa
lengo la kuficha chanzo chake.
Katika
shtaka hilo la sita la kutakatisha fedha Ndama anadaiwa kuwa kati ya
Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini
pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited na akaunti
ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye benki ya Stanbic alijihusisha
moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa
huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa
njia ya udanganyifu.
Ndama alilikubali shtaka hilo na kukana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Miongoni
mwa mashtaka yanayoendelea kumkabili, Ndama anadaiwa Februari 20, 2014
Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na
sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum
Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboxi manne
ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani
8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited
wakati akijua si kweli.
Pia
anadaiwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati
ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha
kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa
na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda
Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila
jinai yoyote wakati akijua si kweli.
Aidha
anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za
usajili R.28092 akionesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa
ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za
Marekani 8,280,000 kutoka Congo.
Shtaka
lingine anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka
Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionesha kampuni ya Muru
imeyawekea bima maboxi manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.
Anadaiwa
kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya
udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade
TJL DTYL Limited Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya atawapa na
kusafirisha dhahabu hizo. Kesi hiyo itatajwa Juni 16,2017.
No comments:
Post a Comment