WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameipongeza timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa kuipeperusha vema
bendera ya Taifa katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika.
“Mwenye
macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na
kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa. Hakika kwa mpira mzuri
wanaocheza wanakonga nyoyo ya mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu
nchini.”
Ametoa pongezi hizo leo (Jumatano, Aprili 6, 2022)
alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na
Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma.
“...Nitumie
fursa hii kuendelea kusisitiza umuhimu wa michezo kwa kuvipongeza
vilabu vyetu vya mpira wa miguu vinavyoshiriki kwenye mashindano ya Ligi
Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) na Ligi Kuu Zanzibar (PBZ
Premier League).”
Pia, Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji mahiri
wa vilabu mbalimbali vya mpira wa miguu nchini vikiwemo Yanga - Timu ya
Wananchi; Simba - Wekundu wa Msimbazi; Namungo - Wauaji wa Kusini; Azam
- Wazee wa Lambalamba.
Vilabu vingine ni Biashara United -
Wanajeshi wa Mpakani; Dodoma Jiji - Walima Zabibu; Tanzania Prison –
Wajelajela; Mtibwa Sugar - Wakata Miwa na Kagera Sugar – Wanankurukumbi;
KMKM, Mlandege, Malindi, Mafunzo na vilabu vinginevyo.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya jitihada mbalimbali
kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua.
Amesema lengo
ni kuimarisha michezo, sanaa na utamaduni ili ziweze kuchangia vema
katika Pato la Taifa sambamba na kuzalisha ajira kwa vijana, kutangaza
utalii, kuimarisha umoja wa kitaifa na afya za Watanzania.
“Nitumie
fursa hii kuwapongeza kwa dhati wanamichezo wote ambao wameiletea
heshima nchi yetu kwa kupeperusha bendera nje ya nchi.” Tuna timu za
mpira wa miguu, ngumi na wasanii mbalimbali.”
Kwa upande wa
mchezo wa ngumi, Waziri Mkuu amewapongeza wanamasumbwi Hassan Mwakinyo,
Tonny Rashid, Twaha Kiduku na Ibrahim Class kwa ushindi mnono
uliowawezesha kupata mikanda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa
waliyoshiriki.
“Nitumie fursa hii pia kuzipongeza timu za mpira
wa miguu za wanawake kwa ushindi wao katika mashindano mbalimbali ya
kimataifa. Kipekee, niwapongeze Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars)
kwa kutwaa ubingwa katika mashindano ya COSAFA mwaka 2021.”
Vilevile,
Waziri Mkuu ameipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Watu wenye
Ulemavu (Tembo Warriors) kwa kufuzu mashindano ya dunia yatakayofanyika
Oktoba, 2022 nchini Uturuki. “Hii ni mara ya kwanza Timu ya Taifa
kushinda na kushiriki moja kwa moja mashindano ya dunia.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha
ujenzi wa Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Wasanii na Wadau wa Sanaa na
kuboresha mfumo wa usajili kwa njia ya kielektroniki.
Amesema
mfumo huo, umewezesha wabunifu 485 na kazi zao 2,921 kusajiliwa, na
Serikali imewezesha wasanii wa fani ya muziki ambao kazi zao zimetumika
kwenye vituo vya redio na televisheni kupata mirabaha. “Nitoe wito kwa
wasanii wote nchini kujisajili katika mfumo huo ili kupata manufaa
tarajiwa.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuliomba
Bunge liidhinishe shilingi bilioni 148.89. Kati ya fedha hizo shilingi
bilioni 101.36 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni
47.52 ni kwa ajili matumizi ya maendeleo. Vilevile, Waziri Mkuu
ameliomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 132.72 kwa ajili ya Mfuko
wa Bunge. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127,32 ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.40 ni kwa ajili matumizi ya
maendeleo.
Post Top Ad
Your Ad Spot
Wednesday, April 6, 2022
SIMBA INAUPIGA MWINGI KIMATAIFA-MAJALIWA
Tags
MICHEZO#
Share This
About kilole mzee
MICHEZO
Labels:
MICHEZO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment