WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt.Pindi
Chana ameziagiza wizara, halmashauri na taasisi nyingine za umma
kuendelea kuitumia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa ajili ya
kuchapisha nyaraka muhimu za Serikali.
Mheshimiwa
Dkt.Chana ameyabainisha hayo leo Machi 18,2022 baada ya kutembelea
Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali iliyopo Keko jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na idara hiyo na
kusikiliza changamoto zilizopo ili Serikali ione namna ya kuzipatia
ufumbuzi.
Amesema,lengo kuu la idara hiyo ni kutoa huduma za uchapaji kwa wakati, kwa kuzingatia ubora na kwa gharama nafuu.
Pia
amesema, idara hiyo inaongozwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ambaye
husimamia vitengo vya Udhibiti wa Ubora, Uzalishaji, Ufundi, Masoko na
Maduka ya Vitabu ya Serikali ina umuhimu mkubwa nchini, hivyo kwa
umuhimu huo taasisi hizo zinapaswa kuitumia kwa maslahi mapana ya Taifa.
Ofisi
ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuchapisha
nyaraka mbalimbali za Serikali ikiwemo sheria mbalimbali na Gazeti la
Serikali ambapo machapisho yake huyauza kupitia maduka ya Serikali
(government shops).
Mheshimiwa
Balozi Dkt.Chana amewashauri wafanyakazi wa idara hiyo kuendelea
kuchapa kazi kwa bidii, uaminifu na uzalendo wa hali ya juu kwa kuwa
jukumu wanalotekeleza Serikali inalithamini na itaendelea kuwa nao
karibu.
"Endeleeni
na uzalendo wenu huu, licha ya uchache wenu nimeshuhudia namna ambavyo
mnafanya kazi kubwa, tena kwa bidii. Hii ni hatua njema sana, Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inathamini sana mchango wa
wafanyakazi katika kulijenga Taifa letu, nanyi ni sehemu ya kundi hilo,
tupo pamoja nanyi na kazi iendelee,"amesema.
"Nirejee
tena wito wangu kwa wizara zote, halmashauri na taasisi nyingine za
umma ziendelee kutumia idara hii kwa ajili ya kuchapisha nyaraka muhimu
za Serikali. Hii idara ni tegemeo kubwa sana kwa Taifa letu, mfano
tunapoelekea katika Sensa ya Watu na Makazi pamoja na Anuani za Makazi,
idara hii inafanya kazi kubwa sana,"amesema Waziri Balozi Dkt.Chana.
Pia
amewataka kuendelea kutumia zaidi malighafi zinazozalishwa hapa nchini
kwa ajili ya uchapishaji na pale inapolazimika kwa kuona malighafi hizo
hazipatikani ndipo utaratibu ufuatwe kwa ajili ya kuagiza nje.
"Tuendelee
kuzitumia kwa wingi malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa ajili ya
kufanikisha uchapaji, ninaamini malighafi hizo zinapatikana, na pale
ambapo itaonekana hazipatikani, baada ya kutafiti kila mahali nchini,
ndipo utaratibu ufuatwe kwa ajili ya kuagiza nje. Tukifanya hivyo,
tutaendelea kukuza uchumi wetu na kuwainua wazalishaji waliopo hapa
nchini kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla,"amesema Balozi
Dkt.Chana.
Maktaba
Akiwa
katika Maktaba ambayo pia inasimamia Duka la Nyaraka za Serikali,
Waziri Balozi Dkt. Chana ameelezwa na Mpiga Chapa Msaidizi Mkuu, Bw.
Alistid Wanyuke kuwa, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,
Serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuanza kutunza nyaraka hizo kwa mfumo
wa kidigitali na kuondoka katika analojia.
Mfumo
ambao, Bw.Wanyuke amesema, ni hatari zaidi hususani katika kipindi hiki
ambacho majanga ya moto yamezidi kuwa changamoto katika maeneo mengi.
"Ninaiomba
Serikali itenge bajeti kidogo kwa ajili ya kufanikisha mfumo wa kuweka
nyaraka za Serikali katika mfumo wa kidigitali na kuondoka huku kwenye
analojia ambapo tunatunza kwa njia za kawada, itasaidia sana kukabiliana
na changamoto za maafa mfano ya moto,"amesema.
Pia
amesema kuwa, kwa sasa duka la nyaraka za Serikali lililokuwa katikati
ya jiji la Dar es Salaam kwa sasa wanaweza kupata huduma hiyo katika
Duka la Nyaraka za Serikali lililopo katika Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali, Keko jijini Dar es Salaam.
Waziri aguswa
Wakati
huo huo, Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana amesema, wazo la kuingia
katika mfumo wa kidigitali kwa ajili ya kutunza nyaraka za Serikali ni
jambo muhimu na la msingi.
Amesema, wataangalia namna ya kushirikiana na wenzao wanaosimamia mfumo huo ili kuona namna ambavyo hilo litafanyiwa kazi.
Balozi
Dkt.Chana ameelezwa kuwa,mfumo huo ukisimamiwa vizuri unaweza pia kuwa
njia rahisi kwa wananchi kununua kupitia mtandao nyaraka hizo kadri
wanavyozihitaji.
Kitengo cha Usanifu
Katika
hatua nyingine, Mpiga Chapa Msaidizi Idara ya Usanifu, Bi.Catherine
Joseph amemweleza Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana kuwa, wanakabiliwa
na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi pamoja na vitendea kazi vya
kisasa ili kuongeza ufanisi katika kazi.
"Mheshimiwa
Waziri, changamoto yetu hapa ni upungufu wa wafanyakazi ambao
unachangiwa na baadhi kustaafu au wengine kufariki. Vile vile tuna
mahitaji ya vitendea kazi mfano printers za kisasa ambazo zikipatikana
zitasaidia kuongeza ufanisi katika kazi,"amesema Bi.Joseph.
Hata
hivyo, Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana amesema kuwa, wamezipokea
changamoto na maoni ya wafanyakazi katika idara hiyo na watazifanyia
kazi hatua kwa hatua ili kuongeza ufanisi katika idara hiyo.
No comments:
Post a Comment