A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, February 10, 2022

STAMINA YA MHESHIMIWA NEEMA LUGANGIRA

 


Adeladius Makwega,DODOMA


Siku ya Ijumaa Februari 4, 2022 nilipata wasaa wa kuingia katika kamati mbili za Bunge nazo ni ile Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na ile Kamati ya Maendeleo ya Huduma za Jamii. Nikiwa katika kamati hizo mie nilingia kwa taaluma yangu tu, maana msomaji wangu usijiulize ukadhani mwanakwetu kapata kitengo la hasha sijakipata.

Maana kwetu Mbagala Mbuyuni na kule Ketaketa kuna nogwa, wasije watu wakapiga hodi nyumbani wakisema kuwa mambo yangu mazuri la hasha, mie choka mbaya.

Kwa kuwa nilikuwa sijaingia katika viwanja hivyo vya Bunge kwa muda mrefu sana maana mara ya mwisho ilikuwa 2014 nilikwenda kama mtayarishaji wa vipindi vya Leo Katika Bunge, Lililojili Bungeni, Mjadala wa leo na Matangazo ya Moja kwa Moja ya Bunge ya TBC Taifa, wakati huo kabla Bunge live halijapigwa mkasi.

Kutoka TBC Taifa Dar es Salaam watangazaji tuliokwenda nao alikuwa Mpendwa Mgweno, mimi na Zaina Katongo (TBC Dodoma). Injinia aliyekuwepo alikuwa ni Omari Salumu akisaidiwa na Fundi Mitambo Josephy Kanyeto (Huyu tulimkuta Dodoma).

Kwa hiyo tangu niingie katika viwanja hivyo sasa inakaribia miaka 9. Baadhi ya Wabunge ambao tulifanya nao vipindi hivyo alikuwemo Bi Pauline Gekul ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa CHADEMA wa Babati Mjini pia mheshimiwa Hendry Shekifu ambaye wakati huo alikuwa wa Mbunge wa CCM kutoka Lushoto.


Hayo yalikuwa ya 2014, ya 2022 ni yepi?

Nilipofika katika viwanja hivyo nilisogelea kibanda cha ukaguzi, nilikaguliwa vizuri lakini kila nilipopita milio ya hatari ililia, basi nilikaguliwa tena na jamaa hawa wa ulinzi kwa kifaa maalumu nadhani viatu vyangu vilikuwa na misumari kwa ndani.

Kwa nyuma yangu alikuwepo Gidion Malabeja huyu ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasimali Watu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kiungwani kwa kuwa tulikuwa safari moja, nilimngonja ili tuingie sote.

Nikiwa namngonja ndugu huyu, mara nilimuona ustadh mmoja ambaye wajihi wake nilikuwa nikiufahamu, yeye hakukaguliwa kama sisi, alipita zake na kuingia katika lango hilo la Bunge akiwa ameshika mkoba. Nilijiuliza mbona ustadh hakukaguliwa? Kumtazama vizuri kumbe alikuwa ni Mbunge wa Lushoto Shabaan Shekilindi.

Nikatambua kuwa hawa waheshimiwa wana utaratibu wao wa kukaguliwa. Kwa kuwa mheshimiwa Shabaan Shekilindi niliwahi kufanya naye kazi, nilimsalimu maana mara ya mwisho kumuona ilikuwa 2018 na nikapiga naye picha nayeye kuelekea katika kikao cha kamati yake.

Mimi nilibaki pale pale kumsubiri ndugu Malabeja ambaye alikuwa bado anakaguliwa maana kila akiingia, ile mashine inalia tu, naona alitoa mkanda mashine ikalia, akavua hadi viatu mashine hii ililia tena, baadaye akapita pekupeku na kukaguliwa tena huku mimi nikimuonea huruma ndugu yangu huyu, baadaye alipita, nikasema kweli Bunge letu ulinzi wake ni madhubuti.

Tulipopita hapo tuliingia katika kamati, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ndiyo ilikuwa ya kwanza kubisha hodi, tulikaribishwa chini ya Makamu Mwenyekiti wake Kilumbi Ngenda na siye tukiongozwa na Bi Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo na Naibu Katibu Mkuu Said Yakubu.

Katika Kamati hii nilivutiwa mno na namna Makamu Mwenyekiti wake Kilumbi Ngenda alivyokuwa akiongoza, huku wakiyasimamia mambo ya Watanzania wanyonge kwa kina, nayo timu ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikijibu hoja hizo kwa ustadi.

Nilifurahi mno katika kamati hii maana nilikutana na Makamu Mwenyekiti Ngenda ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye mwaka 2005-2007 niliwahi kufanya naye kazi huko Iringa na hata Katibu wa Kamati hii pia.

Hapa hoja kubwa za makabwela kadhaa na hoja juu ya Vibanda Umiza vilitetewa mno na mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini na mheshimiwa Polepole.

Tulipomaliza kamati hiyo tulifunga safari hadi Kamati ya Huduma za Jamii, hapa nilizitazama sura zote za wajumbe zilikuwa ngeni, japokuwa kamati hii ilikuwa na wajumbe wengi. Kamati hii nilibaini ilikuwa na waheshimwa wajumbe wenye taaluma mbalimbali huku wakiwa na hoja nzito, chini ya Makamu Mwenyekiti wake Aloyce Kimamba.

“Siyo mchezaji wa timu ya taifa anapigwa kikumbo kidogo anaanguka kule, nashauri suala la lishe liingizwe katika timu zetu ili wachezaji wetu wawe na nidhamu ya chakula, tuna wataalamu wa lishe wengi wawepo katika timu zetu ili wachezaji wawe na stamina na hili lianze tangu wachezaji wakiwa wadogo.”

Mjumbe huyu alikuwa dada mmoja mrefu, mweusi, aliyekata nywele zake, mwenye mwili uliojengeka. Nilipata hamu ya kumfahamu zaidi mbunge huyu, nilimsogelea katibu wa pembeni wa kamati hii mama mmoja mweupe hivi, nikamuuliza jina la mjumbe huyu na bila ajizi alijibu kuwa ni mheshimiwa Neema Lugangira.

Ndipo nikamkumbuka, ahaa kumbe yule mbunge mwenye ajenda ya kudumu ya HAMIROJO (Protein), WANGA (Starch), MAFUTA (Fat), MAZIWA (Dairy) na MATUNDA&MBOGA ZA MAJANI(Fruits & Vegetables),wengine wakimuita mama sayansi kimu/mama chakula bora.

Nilimtazamna mheshimiwa huyu na ajenda yake ya lishe, nia yangu ni kuhakikisha kuwa kama kweli mheshimiwa huyu, je anayaishi anayoyasema? Je yeye mwenyewe ana stamina? Kwa kumtazama nilimuona mheshimiwa huyu ana stamina na ni mtu wa mazoezi.

Mwanakwetu, nilijiuliza je stamina inapimwa kwa kumtazama mtu kwa macho? Nikapata jibu hapana. Nikaona umuhimu wa kuipima stamina ya mheshimiwa huyu kwa mchezo wowote ule atakaouchagua mheshimiwa mwenyewe.Nikasema kuna haja ya kuomba pambano la kupima stamina na mheshimiwa huyu.

Binafsi nimeshajiandaa na pambano hilo maana mama yangu alinilisha lactogen na buruga za kutosha nikiwa mdogo na kwa sasa vyakula vyenye hamirojo, wanga, mafuta, maziwa na mboga za majani & matunda ninazokula zinanipa uhakika wa kushinda pambano hilo la kupimana ubavu.

Refa naomba awe mwalimu Aloyce Kimamba ambaye ndiye makamu mwenyekiti wa kamati hii.

Nilijiuliza swali kama ajenda ya Mheshimiwa Lugangira ni Lishe na mie mwanakwetu ajenda yangu ni kupima stamina ya mheshimiwa huyu, Je wewe ajenda yako ya kudumu ni nini?

Tafakari hilo mwanakwetu, hakikisha kuwa kila unalolifanya uwe na ajenda yako ya kudumu. Nakuuma sikio kuwa ajenda ya kunichagulia mchezo wa kupimana stamina na mheshimiwa Lugangira sitaki, hiyo ni kazi ya mheshimiwa Lugangira pekee, kwanza apokee ombi hilo na pili akubali na tatu achague mchezo wa kupimana stamina.

Nikiwa bado kikaoni, mara nilimsikia mheshimiwa Pauline Gekul Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo akisema,

“Mheshimiwa mwenyekiti tunashukuru sana kwa ushirikiano wenu na haya yote tuliyoyajibu tutayaleta kwa maandishi.”

Kikao kiliisha wakubwa walisimama na mie kusimama na kutoka nje ya ukumbi huu na mie kurudi zangu madongo poromoka, huku mvua kubwa ikinyesha.


makwadeladius@gmail.com

0717649257 




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages