MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa wafanyabiashara kutumia fursa za rasilimali zilizopo kuwekeza katika uzalishaji wa viwanda.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo huko Viwan vya Masira mjini Zanzibar alipofungua tamasha la nane la maonesho ya biashara Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za kutimia miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amefahamisha kwamba viwanda vinavyoanzishwa ni vyema vilenge katika kuzalisha bidhaa bora zinazozingatia viwango vya kimataifa kwa kusarifu na kuongeza thamani ya bidhaa hizo kwa uzalishaji wa mafuta, arki na dawa zinazoweza kutumika kwa masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Aidha amesema kwamba kunahaja kwa wizara inayoshughulikia masuala ya biashara na maendeleo ya Viwanda Zanzibar kuwa na mkakati madhubuti wa kuhamasisha jamii kupenda kununua na kutumia bidhaa za ndani.

Kwa upande mwengine, Mhe. Othman ameshauri kukutanishwa wadau wa biashara na maendeleo ya kiuchumi ili kubadilishana mawazo kwa nia ya kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Amesema hatua hiyo pia ni kutoa nafasi kwa wadau wa biashara, viwanda, kilimo na utalii kwa pamoja waweze kubaini fursa mpya za kiuchumi zilizopo sambamba na kutambua huduma zinazotolewa zilivyoboreshwa ikiwa ni jitihada za kuharakisha maendeleo nchini.

Aidha Mhe. Makamu ameshauri kwamba ni vyema tamasha hilo la biashara kutoka ngazi ya kitaifa na kikanda hadi kuwa ya kimataifa ili watu wengi zaidi waweze kujumuika katika kujionea na kutumia fursa za biashara na kiuchumi na hivyo kuharakisha kuleta maendeleo ya taifa.

Mapema Mhe. Othman alitembelea mabanda mbali mbali ya maonesho katika tamasha hilo na kujionea juhudi mbali mbali za uzalishaji wa bidhaa za viwanda na huduma zililizpo katika maonesho hayo.

Naye waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shabani amesema kwamba tamasha hilo limechangia sana kuabadilishana uzoeifu na kuongeza uzoefu sambamba na kupunguza changamoto ya masoko kwa wafanyabiashara.

Aidha amewataka wajasiriamali wote nchini kujisajili katika mamlaka na taasisi mbali mbali zilizomo katika wizara hiyo kwa lengo la kutambuliwa na kuwezeshwa kutumia vyema huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghabi Idrisa Kitwana Mustafa amesema kwamba tamashga hilo ni fursa muhimu kwa wafanyamiashara kujifunza masuala na kubadilishana uzoeifu na wajasiriamali wengine kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Dk. Islam Seif Salim mesema kwamba tamasha hilo limepata maendeleo makubwa kutokana na kuongezeka kwa washiriki hadi kufikia 374 ambapo miongoni mwao ni wa nje uya nchi.

Tamasha hilo la maonesho ya biashara limezishirikisha taasisi za serikali na binafsi pamoja na wazalishaji wa bidhaa mbali mbali na ni la nane tokea kuanzishwa kwake hapa Zanzibar