Na Mwandishi wetu, Dar es Saalam | KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo kwa kuzingatia kundi la watu wenye ulemavu kwa kulijumuisha, kulishirikisha na kuliwezesha.
Shaka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana mbele ya wajumbe na viongozi wa KISUVITA.
Alisema serikali chini ya CCM imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaheshimiwa, kuthaminiwa, kushirikishwa, kulindwa na wanajumuishwa katika mipango ya maendeleo katika jamii.
Alibainisha kuwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022, serikali imetenga sh. bilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa visaidizi kwa wanafunzi katika shule zote za wenye ulemavu nchini.
“Kundi hili limeendelea kunufaika na fursa ya mikopo isiyo na riba inayotokana na asilimia mbili ya mapato ya ndani ya halmashauri zetu,” alisema.
Hata hivyo, alisema serikali imeelekeza wenye ulemavu wawezeshwe kupata taarifa kulingana na mahitaji ya kundi husika, ikiwemo kuwekewa wataalamu wa lugha za alama na maandishi ya nukta nundu.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuwaheshimu, kuwathamini na kuwaunga mkono wenye ulemavu katika kila eneo wanaloshiriki kama ilivyo kwa watu wasio na ulemavu.
Kwa mujibu wa Shaka, taasisi na mashirika ya kibiashara yanapaswa kujitokeza kudhamini programu za michezo, sanaa, uchumi na utamaduni, kwani kufanya hivyo ni kuunga mkono dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga nchi yenye usawa.
Aliwapongeza kwa hatua ya ushindi katika mashindano waliyoshiriki nchini na Urusi, kwani wameiheshimisha Tanzania.
Shaka aliongeza kuwa Katiba ya CCM katika imani imeeleza kwamba binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake, pamoja na haki zote za msingi bila kubaguliwa.
Alisema mkazo huo umekwa hata katika Katiba ya nchi, ambapo imebainisha kuwa italinda haki za watu wenye ulemavu na serikali iliandaa sera ya fursa kwa kundi hilo ya mwaka 2004.
“Pia Tanzania imeridhia mikataba na maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu haki na usawa wa fursa kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali,” alisisitiza.
Aliweka wazi kuwa hata Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 imesisitiza serikali kukabiliana na mitazamo hasi na mila potofu dhidi ya watu wenye ulemavu ili kujenga jamii yenye usawa na fursa kwa wote.
Katibu huyo wa NEC, alibainisha kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban asilimia 10 ya idadi ya watu duniani wana aina fulani ya ulemavu na asilimia 80 kati yao wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 nchini, idadi ya wenye ulemavu Tanzania ni watu 2,641,802.
“Tanzania ni moja kati ya nchi zinazofanya vizuri duniani katika upatikanaji wa taarifa na takwimu za wenye ulemavu, na hizi zinasaidia kuweka misingi madhubuti katika kupanga na kutekeleza programu mbalimbali za kuboresha maisha yao,” alisema.
No comments:
Post a Comment