Na Yusuph Mussa, Lushoto

MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu 'Bosnia', akishirikiana na wananchi wa Kitongojji cha Mheza, Kijiji cha Lwandai, Kata ya Mlola, wametengeneza daraja la muda ili kuwasaidia wananchi wa kata tatu za Kilole, Kwekanga na Mlola zenye zaidi ya wananchi 60,000 kuwa na mawasiliano.

Ni baada ya daraja hilo lililojengwa zaidi ya miaka 20 kuweza kusombwa na maji Novemba 27, mwaka jana, na kusababisha adha kubwa kwa wananchi, na kushinda kufanya shughuli za maendeleo kwa magari kushindwa kuvuka upande wa pili, huku wagonjwa wakibebwa na bodaboda kupelekwa Kituo cha Afya Mlola.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga Shaaban Shekilindi maarufu 'Bosnia' (wa tano kushoto), akiwa ameshika sululu kuchimba njia ya kulitoa karavati ili kulipeleka kwenye daraja la muda. Makaravati hayo yalisombwa na maji Novemba, mwaka jana. (Picha na Yusuph Mussa).

Kazi ya kuchukua makaravati yaliyosombwa na maji na kuyapanga upya kwa ajili ya daraja la muda, ilifanyika Julai 24, 2021 huku viongozi wa Kata ya Mlola, Kijiji cha Lwandai na Kitongoji cha Mheza wakishirikiana na wananchi na Mbunge. Na walifanikiwa kupanga, na kazi hiyo imekamilika Julai 25, 2021 baada ya kujaza mchanga viroba 120 ili kufanya magari yaweze kupita.

"Daraja hili lilikuwa linanilaza macho hasa nikifikiria wananchi wa kata tatu za Kwekanga, Kilole na Mlola wakikosa mawasiliano na kazi zao kuzorota. Hivyo nikaona, wakati tunasubiri fedha za Serikali ziweze kufika, ambapo katika sh. milionii 500 tulizopewa na Serikali kufanyia matengenezo ya barabara na daraja hili lipo, basi tuanze kutengeneza wenyewe kwa kutumka nguvu zetu.

"Na kwa magari kuanza kupita hapa, kutatoa fursa nyingi za kiuchumi, kwani wakati wananchi wengine wa kata ya Mlola wanauza kokoto, mawe na mchanga kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Lushoto kinachojengwa Mlola, wananchi wa vitongoji vinne vya Kijiji cha Lwandai wao walikuwa hawapati fursa hiyo kwa vile magari yalikuwa hayapiti upande wa pili. Hivyo kwa kukamilisha daraja hili, sasa uchumi wa wananchi wa Mheza na wenzao wataingia kwenye shughuli za kiuchumi," alisema Shekilindi.
Alisema, katika suala la barabara, Serikali ya Awamu ya Sita imempendelea, kwani katika mwaka wa fedha 2021/2022, imeweza kumpa sh. bilioni tano. Katika fedha hizo, sh. bilioni 3.5 zitatumika kutengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Mlalo- Mlola- Makanya- Milingano- Mashewa yenye umbali wa kilomita 70. Na sh. bilioni moja ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto hadi Ofisi za Halmashauri Lushoto, na sh. milioni 500 ni matengenezo ya sehemu korofi kwa jimbo zima la Lushoto.

Akisikiliza kero za wananchi mara baada ya msalagambo huo wa ujenzi wa daraja kukamilka, Shekilindi alisema tatizo la maji kwenye vijiji vya Mazashai, Ungo, Lwandai, Mbula, na kata nzima ya Mlalo litabaki historia, kwani tayari Serikali imetenga fedha sh. milioni 90 kwa ajili ya mradi wa maji kwenye kata hiyo.

Shekilindi alisema pamoja na miradi ya maji safi na salama, pia kutakuwa na miradi ya ujenzi wa mabwawa ili wananchi waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji wa mbogamboga, huku wakipata maji safi wakati wote, huku akisema kuna mradi mkubwa wa maji unakuja wa kata 13 kati ya kata 15 za jimbo hilo wenye thamani ya sh. bilioni 16.
Kuhusu suala la mawasiliano ya simu kwa baadhi ya vitongoji vya kata ya Mlola ikiwemo kitongoji cha Mheza, Shekilindi alisema anafanyia kazi ili wananchi waweze kuwa na mawasiliano ya uhakika ili kurahisisha huduma za kijamii ikiwemo za kifedha.

Awali, Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Mlola Bakari Kodema alisema tatizo la maji na mawasiliano, bado ni changamoto kwa baadhi ya vijiji na vitongoji vya kata hiyo, hivyo anaomba Mbunge aendelee kuchagiza ili wananchi wapate huduma hiyo.