Msimu wa 12 wa mbio za Rock City Marathon zinazofanyika kila mwaka jijini Mwanza umezinduliwa rasmi hii leo jijini humo huku serikali ikiahidi kuendelea kutumia mbio hizo kuibua vipaji vya mchezo wa riadha sambamba na kutangaza utalii wa ndani.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bw Hassan Elias Masala aliekuwa akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel alisema ni nia ya serikali kuona mashindano hayo yanakuwa chachu ya kuwezesha kupatikana wanamichezo watakaoweza kushiriki katika Mashindano ya Kitaifa na Kimataifa.


“Ili agenda kuu ya kutangaza utalii wetu iweze kufanikiwa ni wazi kwamba lazima tuwe na matukio yanaweza kuwashawishi wenzetu kutoka nje waje kututembelea. Uwepo wa mashindano makubwa kama haya ndio utatuwezesha kufanikisha hili, hivyo nawasihi wadau wote tujitokeze kuunga mkono mbio hizi,’’ alisema Bw Masala ambae pia aliahidi kushiriki mbio hizo.


Mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Octoba 24 kwenye viunga vya jengo la biashara la Rock City Mall, jijini humo tayari zimefanikiwa kuvutia wadhamini na wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni ya TIPER, Serengeti Breweries, Benki ya KCB, Kampuni ya Uhandisi ya Magare, Pepsi,Maji ya Uhai, Rock City Mall, Kampuni ya Ulinzi ya GardaWorld,  Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Azam tv  na CF Hospital.


Zaidi alitoa wito kwa wadau na wakazi kutoka ndani na nje ya jiji hilo kuhakikisha wanashiriki katika matukio mbalimbali yatakayo ambatana na mbio hizo ikiwemo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo kanda ya Ziwa, kushiriki mbio zenyewe pamoja na kuwa sehemu ya wadhamini wa mbio hizo.


Kwa upande wake Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bw Kasara Naftal alisema maandalizi yanaendelea vizuri huku akibainisha kuwa lengo haswa ni kukimbiza washiriki zaidi ya elfu tano.


“Tunajitahidi kufanya maandalizi ya kutosha na yenye kufuata viwango vya kimataifa ili kuwawezesha washiriki wa mbio hizi wakiwemo wale wa kimataifa wapate wasaaa wa kushiriki kikamilifu bila vikwazo vya aina yoyote.’’


“Hili pia huwa tunalifanya makusudi ili washiriki hawa wakawe mabalozi wazuri wa mbio hizi pamoja na malengo ya kuanzishwa kwake kwa maana ya kutangaza utalii pindi wanaporudi katika mikoa na mataifa yao hasa kwa wale wanaotoka nje ya nchi.’’ Alisema.


Mbali na mbio za km 21, mbio za Rock City Marathon pia zinatarajiwa kuhusisha  makundi mengine ya mbio ambayo ni pamoja na mbio za kilomita 10 kwa wanaume na wanawake, kilomita 5 kwa ngazi ya ‘corporate’ na watu wenye ualibino pamoja na watoto wenye umri kuanzia miaka 7.


Kuhushu usajili wa mbio hizo Bw. Naftal alisema unatarajiwa kuanza rasmi Julai mosi mwaka huu kwa njia ya mtandao.


Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bw Hassan Elias Masala (alieshika mkasi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa msimu wa 12 wa mbio za Rock City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Octoba 24 mwaka huu kwenye viunga vya jengo la biashara la Rock City Mall, jijini Mwanza wakati wa hafla maalum ya uzinduzi wa mbio hizo iliyofanyika jijini humo leo. Wanaoshuhudia ni wadau mbalimbali wa mbio hizo wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa mchezo wa huo,  wadhamini na waandaaji wa mbio hizo.


Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bw Hassan Elias Masala  akizungumza kwenye hafla hiyo.


Mratibu wa mbio za Rock City Marathon  kutoka kampuni ya Capital Plus International, Bw Kasara Naftal akizungumza kwenye hafla hiyo.


Rock City Marathon mbio za makundi yote! Wadau wa Rock City Marathon.


Mkuu wa wilaya ya Ilemela Bw Hassan Elias Masala (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa mbio za Rock City Marathon wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa mchezo wa huo,  wadhamini na waandaaji wa mbio hizo.


Baadhi ya wadau wa mchezo wa Riadha jijini Mwanza wakiwa kwenye uzinduzi wa mbio za Rock City Marathon msimu wa 12.