Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amekutana na Viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited wakiongozwa na Kaimu Mtendaji Mkuu Bw. Bakari Machumu kujadili namna Kampuni hiyo itakavyo shirikiana na Serikali kufikia dira ya maendeleo ya nchi.
Ziara Viongozi hao imefanyika leo April 20, 2021 katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jengo la PSSSF Jijini Dodoma ambapo wamefanya mazungumzo na Waziri mwenye dhamana ya Habari Mhe. Bashungwa.
Waziri amesisitiza kuwa Wizara yake itaanzisha programu shirikishi ya kuwaita Wahariri wa Vyombo mbalimbali nchini kuwajengea uelewa wa pamoja kwa kutembelea miradi inayotekelezwa wajionee wenyewe na kuuhabarisha Umma juu ya miradi inayotekelezwa na kusimammiwa na Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Waziri Bashungwa ameongeza kuwa Vyombo vya Habari ni vinara katika kulipeleka Taifa mbele kiuchumi kwa kutangaza fursa zilizopo nchini kutokana na historia ya Tanzania Barani Afrika ya kuongoza mapambano ya kulikomboa Bara hilo.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Bakari Machumu ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutangaza fursa na miradi mbalimbali inayotekelezwa Serikali hatua inayowasaidia kupata waandishi wa habari na watangazaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Machumu ameongeza kuwa Uongozi wa Kampuni hiyo umefurahishwa na Serikali kuwa tayari muda wote kutoa ushirikiano mara zote wanapohitaji kupata taarifa katika maeneo mbalimbali hatua inayowaidia kuwa wa kwanza kuzungumzia miradi inayotekelezwa na Serikali.
Kampuni ya Mwananchi ni miongomi mwa taasisi zinazochapisha Magazeti nchini ambapo inamiliki magazeti matatu ambayo yamekuwa chanzo cha habari kwa wananchi kupitia magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
No comments:
Post a Comment