Benki ya NMB imezindua huduma mpya tatu za kidigitali zenye lengo la kurahisisha mawasiliano kati yao na wateja na kuwapatia wateja wake huduma bora kwa wakati.
Huduma hizi – zilizotambulishwa chini ya kampeni ya tatu za kibabe – zimezinduliwa wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja duniani iliyoanza leo na kuhitimishwa Ijumaa 09 Oktoba 2020.
Huduma hizi tatu mpya ni namba maalumu ya huduma kwa wateja ya WhatsApp ambayo ni +255 747 333 444. Hii ni namba kwa ajili ya mteja anayetaka ufafanuzi wa huduma za benki.
Huduma ya pili ni QR Code, ambayo inatoa nafasi kwa wateja kutoa maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za kibenki za NMB.
Huduma ya tatu, ni huduma ya kurudisha token ya LUKU kwa mteja ambae amenunua umeme kupitia NMB Mkononi na hajaipata, basi ataweza kuipata mara moja kwa teknolojia ya matamshi. |
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (wa pili kulia) akizindua huduma mpya 3 za kibabe za NMB, katika hafla iliyofanyika katika Makao Makuu wa Benki hiyo jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna (mwenye nguo nyekundu), Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (kulia) pamoja na wafanyakazi wa NMB.
|
Huduma ya namba ya WhatsApp itasaidia kuwasiliana na wateja kwa muda mfupi kwani mteja ataweza kutuma ujumbe na picha kwenye namba hiyo na kupata majibu ndani ya muda mfupi kabisa. QR Code yenyewe imewekwa kwenye ATM zote za benki hiyo na kwenye madawati ya huduma kwa wateja kwenye matawi ya NMB nchi nzima. Mteja atatakiwa kutumia simu yake janja kwa kumulika (Scan) kwenye QR Code, hapo kisanduku cha maoni kitatokea na mteja ataweka maoni yake ya jinsi alivyopata huduma kutoka NMB. |
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk. Edwin Mhede (katikati), Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (wa pili kushoto), Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja, Abella Tarimo (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Wafanyakazi, Onesmo Kabeho baada ya kuzindua huduma mpya 3 za Kibabe za NMB.
Kwa upande wa huduma ya LUKU, kama mteja amenunua umeme kupitia NMB Mkononi, na hajapata token yake, anaweza kuipata token yake kwa kupiga simu ya bure 0800 002 002, ana chagua 1, tena chagua 1 kuendelea, baada ya hapo ataweka namba yake ya mita na token itatajwa kwa maneno. Mteja wa NMB ataweza kuipata huduma hii akiwa nyumbani au mahala popote na wakati wowote.
Benki ya NMB inakuwa ya kwanza kuja na suluhusho la mawasiliano haswa kwenye token za LUKU hapa nchini. Haya ni maendeleo makubwa na wanajivunia kuwa wa kwanza kutatua kero kama hizi za wateja ili kurahisisha huduma. |
No comments:
Post a Comment