Benki ya CRDB imetangaza udhamini wa shilingi milioni 200 kwa ligi ya mpira wa kikapu ya taifa 2020 itakayofanyika Dodoma katika viwanja vya Chinangali kuanzia tarehe 12 Novemba na kilele chake ni 21 Novemba, 2020.
Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa amesema benki hiyo imefikia makubaliano na Shirikisho la Taifa la Mpira wa Kikapu (TBF) ya udhamini wa ligi hiyo ya taifa ya mpira wa kikapu ambayo imepewa jina la “CRDB Bank Taifa Cup”.
Mwambapa alisema udhamini wa ligi hiyo ya taifa ya mpira wa kikapu ni muendelezo wa jitihada za Benki ya CRDB katika kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupitia michezo. Aliongezea kuwa Benki hiyo kupitia sera yake ya Uwezeshaji katika Jamii (CSI Policy) imekuwa ikiwekeza katika michezo ya vijana kwa kuamini kuwa inasidia kuongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.
Akizungumzia kuhusu msukumo uliopelekea Benki hiyo kudhamini ligi hiyo ya taifa ya kikapu yenye kauli mbiu ya “Ni Zaidi ya Game, Ni Maisha”, Mwambapa alisema mchezo wa mpira wa kikapu umekuwa haupewi sana kipaumbele kulinganisha na michezo mingine, Hivyo kupelekea kiwakatisha tamaa vijana wengi ambao wamekuwa wakionyesha vipaji katika mchezo huo.
“CRDB Bank Taifa Cup” inakuja kuleta hamasa si tu kwa vijana na wapenzi wa mpira wa kikapu bali kwa Watanzania wote kwa kuwaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika michezo ya vijana na fursa zilizopo ikiwamo ajira,” alisema Mwambapa.
Mwambapa alisema mbali na zawadi zitakazokuwa zikitolewa kwa timu zitakazofanya vizuri katika “CRDB Bank Taifa Cup”, Benki ya CRDB pia imetenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya “Scholarship” kwa wachezaji watakaofanya vizuri.
“Tutakuwa pia na zawadi kwa ajili ya wapenzi wa mpira wa kikapu katika kila hatua za mashindano. Niwaombe watanzania waanze kutufuatilia kupitia Azam TV na mitandao yetu ya kijamii kujua namna ya kushiriki,” aliongezea Mwambapa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, Mike Mwita aliishukuru Benki ya CRDB kwa kudhamini ligi hiyo ya taifa ya mpira wa kikapu huku akisema udhamini huo utaongeza mapenzi ya mpira wa kikapu kwa vijana kama ilivyo kwa mpira wa miguu na michezo mingine.
Mwita alisema: "Tunafurahi sana kwa udhamini na ushiriki thabiti wa Benki ya CRDB katika jitihada hizi zinazolenga kukuzwa kwa mpira wa kikapu nchini. Sio tu kwamba udhamini wa Benki ya CRDB utaboresha kiwango cha ligi, lakini pia utavutia Watanzania wengi kufuatilia mchezo huu na kuhamasisha vijana wengi kushiriki."
Naye Msimamizi wa vipindi vya michezo Azam TV, Michael Maluwe amewataka Watanzania kuanza kufuatilia CRDB Bank Taifa Cup kupitia chaneli ya michezo ya Azam Sports 2, ambapo Benki hiyo imeanzisha kipindi maalum kuelekea mashindano hayo ya mpira wa kikapu. “Azam TV itaweka kambi Dodoma kuwaletea burudani Watanzania kuelekea mashindano haya, niwakaribishe Watanzania tujiunge na Azam TV ili kuwashangilia vijana wetu,” alisema Maluwe.
CRDB Bank Taifa Cup inatarajiwa kuhusisha timu 36 za mpira wa kikapu kwa upande wa wanaume na wanawake. Mashindano hayo pia yatatanguliwa na michuano ya timu za veteran zza Benki ya CRDB, Bunge, Pazi, Bahari na timu za walemevu. Pamoja na Benki ya CRDB kuwa mdhamini mkuu, CRDB Bank Taifa Cup pia imedhaminiwa na Azam TV, kampuni ya bima ya Sanlam na kampuni ya maji ya Cool Blue.
No comments:
Post a Comment