A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Sunday, July 26, 2020

WAJUMBE HONGERENI MMETIMIZA WAJIBU WENU MCHAKATO KURA ZA MAONI...WATIA NIA WENGINE WALIKUWA 'WAZINGUAJI TU'

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

NIKIRI nimeamua kuandika hiki ambacho nakiandika baada ya kuona kuna lugha za kejeli ambazo zinatolewa na baadhi ya watia nia ambao wameshindwa kwenye kura za maoni.

Kuna clips ya Video inayosambaa mtandaoni  inayozungumzia kwamba wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wana elimu ya darasa la saba. Katika video hiyo mmoja ya watia nia ya nafasi ya ubunge anasema wajumbe wenyewe wamechoka na wana roho mbaya.

Halafu wajumbe hao hao elimu yao ni darasa la saba na wakiwa  500 ndio wanakuwa na akili. Hayo maneno sio sawa hata kidogo.Labda kama yalikuwa yamejikita kwenye kutania na sio uhalisia.Tuweke vizuri kidogo.

Kwanza lazima tukubali wajumbe wametimiza wajibu wao,wanajua wanachokifanya ,wanajua nafasi yao ilivyo muhimu katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama chao.

Ndio ukweli huo, wajumbe ni binadamu, wanazo akili timamu kama walivyo wengine wakiwamo wa tia ya ubunge na udiwani.Unaposema elimu ya darasa la saba nikuwavunjia heshima.

Sawa lazima tukubali wajumbe hawawezi wote kuwa wasomi wa Chuo Kikuu, au wote wa darasa la saba.Wanaviwango tofauti vya elimu na hiyo siyo dhambi.Wanayo dhamana ya kupiga kura kutokana na utaratibu uliowekwa na Chama chao.Wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa muda mrefu.


Ni wajumbe hao hao ndio wamekuwa wakipiga kura kwa watia nia katika nafasi mbalimbali za ubunge na udiwani.Wamekuwa wakiifanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa.Wanastahili pongezi, na sote tunafahamu katika chaguzi kuna kushinda na kushindwa.

Kabla ya kutoa lawama kwa wajumbe kutokukupa kura jitafakari, je unatosha kuwatumikia wananchi kwa nafasi unayoomba iwe udiwani au ubunge.

Ni muhimu mtia nia kujiuliza katika nafasi unayokwenda kuomba utaifanya kwa uwezo na nguvu zako zote.Kuna baadhi ya watia nia hata ofisi za CCM za kuchukulia fomu hawakuwa wanazijua, akifika kwa bodaboda anamwambia kama unajua ofisi za CCM Wilaya au CCM mkoa ampeleke.

Mtia nia wa aina hiyo akikutana na wajumbe anatarajia nini? Kwanza watia nia wengine walikuwa wanazingua tu.

Unadhani wajumbe  hawajui nani anafaa au nani hafai, unakwenda jimboni kwasababu ya kutaka ubunge tu, wengine wanakwenda vijijini kwao wakati wa msiba na akizika anarudi mjini na gari iliyopeleka mwili wa marehemi.Unatarajia nini?

Unakwenda jimboni kwasababu unataka ubunge,kabla ya hapo hakuna aliyekuona.Wajumbe hawana muda wa kupoteza kabisa.Wanakula kichwa tu, kwanza hawajali maana hawakujui.Hata ukiwapa hela watachukua na kisha kuendelea kusimama na mtu sahihi.Maisha yako Dar es Salaam ikifika wakati wa uchaguzi mkuu ndio unakwenda jimboni.Kha!

Mjumbe hawezi kukuelewa, atachagua anayemuona, anayemthamini na anayejua watakuwa wote wakati wote. Ni kweli Mjumbe anaweza kukosa elimu ya darasani  lakini akawa na elimu ya kutosha ya kuishi na watu.

Wajumbe wanajua namna ambavyo wanakumbana na baadhi ya wasomi waliokuwa na changamoto kibao, Hawajui shida za watu ila wanajali kupigiwa kura. Ikifika wakati wa kuomba kura wanapigana vikumbo majimboni na kwa wajumbe.

Kuna wasomi sio wote ,wameona ubunge kichaka cha utajiri, waamini wakikaa bungeni baada ya miaka mitano akaunti zao benki zitakuwa zimenona. Wanaona kazi nzuri ni ubunge tu. Wajumbe wanakwambia hapana, ubunge ni dhamana,ubunge ni utumishi,ubunge ni kukubali kutumwa,ubunge ni unyenyekevu,ubunge ni kuwaheshimu na kuwajali walio mbele yako.

Ubunge ni kujua changamoto za wananchi unaowawakilisha katika vyombo vyenye maamuzi, ubunge ni utumwa, wananchi wanakutuma kupeleka shida zao ndani ya Bunge.Wajumbe lazima wawe na uhakika na huyo anayeomba ridhaa.

Ndio maana Mbunge wa Geita Joseph Msukuma hana shida na wajumbe, anajua kutekeleza majukumu yake ya kibunge.Akifika kwa wajumbe lazima watampa kura tu,huko mbele ya safari akivurunda hawatampa,ndio ukweli.

Wajumbe wako makini sana, wakati mtia nia unaomba kura wanakuangalia,kisha wanasema huyu wawapi au kapotea njia? Ukiwa naye meno 32 yote nje jinsi anavyokuchekea,mpe kisogo anakwambia huyu naye anajisumbua tu.

Kwa mazingira ya aina hiyo Mjumbe lazima aonekane mbaya, na atapewa kila aina ha jina baya hasa kwa kipindi hiki.Sababu wametimiza wajibu.Wajumbe wanajua watia nia wazuri, unadhani wajumbe waliompitisha Dk.Philip Mpango kwenye kura za maoni wamekosea?

Hapana wako sahihi sana, sote ni mashahidi Dk.Mpango ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango amefanya kazi nzuri ndani ya nchi yetu.

Wajumbe wanajua uwezo wa Mama yangu Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri wa Afya,Maendeeleo ya Jamii,Jinsia , Wazee na Watoto. Mama wa watu anafanya kazi nzuri sana, na leo hii ameshinda kwa kura nyingi kwenye kura za maoni katika Jimbo la Tanga Mjini.

Kuna mifano mingi tu, Jimbo la Kongwa Spika wetu Job Ndugai ameshinda kwenye kura za maoni, kazi ambayo imefanywa na huyu mzee wangu Bungeni sote tunaifahamu,amelisimamia vema Bunge.Pia anawawakilisha vema wananchi wa jimbo la Kongwa. Wajumbe wanawajua vema watia nia kwenye maeneo yao.

Hata walioshindwa kwenye kura za maoni kuna sababu ya kushindwa.Mbunge hana alichokifanya ndani ya miaka mitano iliyopita leo unakwenda kuwaomba kura, ukweli hawatakupa,watakunyima tu.Kwani unalipi kubwa ambalo umewafanyia.Kabla ya kupeleka lawama kwa wapiga kura lazima mtia nia ujitafakari.

Jamani ,wajumbe wanasikiliza sera mtia anakuja na hoja akipewa nafasi na kuwa mbunge ataweka pazia Mlima Kilimanjaro, kwa mazingira ya aina hiyo unategemea wajumbe wafanye nini? Hata ningekuwa mimi sikupi kura.Haki ya Mungu tena.

Wakati naandika hiki ninachoandika, kumekuwepo na madai ya rushwa kutumika kwa kupewa baadhi ya wajumbe na ndio maana wapo walioshinda kura za maoni.

Kwa kuwa hizo ni tuhuma vyombo vinavyohusika vipo.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) ipo na ndio kazi yake hiyo.Toa taarifa na wao watafanya uchunguzi.

Hata hivyo wengi wamekosa kura sio kwasababu ya rushwa,la hasha , kuna sababu zaidi ya hizo.Sio wote lakini wengi wamekosa sifa.Hivi unataka ubunge kwa wananchi na wakati huo huo ndio unapambana kujenga nyumba.Siku zote ulikuwa wapi? Inamaana bila kutaka ubunge usingejenga kwenu.

Wapo watia nia ambao kutwa kucha,wako mitandaoni, na wakiona wamepata umaarufu basi wanajua wakienda majimboni wajumbe watawachagua.Huko ni kujidanganya, wajumbe wanapiga kura kupendekeza watia wenye kujua shida zao na sio watia nia wenye kujua changamoto za bei ya bando la intaneti.

Wananchi wanachangamoto nyingi kuliko intanet kushindwa kupakua wimbo wa Baba Lao wa Diamond Platnuz. Ndio ukweli. Wajumbe wana akili nyingi kuliko unavyowafikiria, unaposimama tu mbele wanajua kabisa hakuna mbunge ,kuna mbabaishaji tu anataka maisha kupitia wao.

Binafsi wajumbe nawapa hongera kwa kazi ambayo mmeifanya,mmeirahisishia Kamati Kuu ya CCM kupata jina moja la mgombea kati yao hao ambao mmependekeza kuanzia wa kwanza , wa pili na watatu. Kuna majimbo watia nia walikuwa zaidi ya 150, wajumbe wakafanya kazi yao na hakika wameimaliza vema,mengine ya Kamati Kuu.Tusubiri.

Ukitaka kujua nguvu ya wajumbe , wale wote ambao huwa wanawachagua na kisha wakaongoza kwa kura,wakikatwa na majina yao na kisha kwenda Chama kingine cha siasa lazima watashinda,unajua kwanini wanajua nani anatakiwa na wananchi.

Rejea chaguzi zilizopita utakubaliana nami.Anakuwa wa kwanza kwenye kura za maoni halafu watu wanapindua matokeo.Yetu macho.Ni matumaini yangu safari hii haki itatendeka na sina shaka na Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Alitaka uwazi kwenye kura za maoni,hakika faida yake tumeiona.Kura zimepigwa hadharani na kuhesabiwa hadharani.Tumeshuhudia na hakika macho na na masikio yetu yameandika historia ya aina yake katika medani za kisiasa nchini kwetu. Wajumbe wote mnastahili kupongezwa kwa kufuata maelekezo.

 Mwisho kabisa ila sio kwa umuhimu nawapongeza watia wote waliochukua fomu.Mbegu mliyopanda kuna siku itaota ,haitapotea,kikubwa tuendelee kushirikiana kuijenga Tanzania yetu iliyozuri.

Kama vipi mtu wangu tutete
basi kwa namba 0713 833822

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages