mwandishi wa habari Angellah Kiwia na dereva Mohamed Rushaka wakitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi laki nne kila mmoja.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mwandishi wa habari Angellah Kiwia na dereva Mohamed Rushaka kulipa faini ya sh. Laki nne kila mmoja ama kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ua kutiwa hatiani kwa kosa kujipatia pesa kwa njia ya vitisho.
Pia mahakama imewaamuru kulipa fidia ya Sh milioni 30 baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchibi (DPP), ya kukiri makosa baina yao.
Hata hivyo, watuhumiwa Kiwia na Rushaka wamefanikiwa kulipa fedha hizo na wameachiwa huru.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Rashid Chaungu ambaye kabla ya kuwasomea hukumu hiyo, aliwafutia washtakiwa hao mashtaka matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakibili.
Mapema kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi Ladislaus Komanya aliiomba mahakama kufanyia mabadiliko hati ya mashtaka na kwamba katika makubaliano yaliyofanywa baina ya washtakiwa na DPP amewafutia mashtaka ya awali yenye makosa manne na kusoma hati mpya yenye kosa moja la kujipatia fedha kwa njia ya vitisho.
Aidha wakili Komanya aliiomba mahakama kutoa adhabu kulingana na makubaliano yaliyoingiwa kati ya DPP na washitakiwa hao.
Awali washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kuwa, kati ya Machi 1 na Machi 31, 2020 katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi washtakiwa waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Katika shtaka la pili washtakiwa hao walidaiwa kutenda kosa la utekaji nyara kati ya Machi 1 na Machi 31, 2020 katika jiji la Dar es Salaam, walimteka Seleman Mohamed wakiwa na lengo kumpeleka katika hatari ya kumuumiza.
Pia ilidaiwa katika shtaka la tatu washtakiwa hao wakiwa na lengo la kulipwa walidai kiasi cha Sh milioni 30 kutoka kwa Seleman Mohamed, huku wakimtishia kumuua.
Aidha katika shtaka la nne la kutakatisha fedha ilidaiwa kuwa washtakiwa hao katika tarehe zilizotajwa awali jijini Dar es Salaam walijipatia Sh milioni 30 kutoka kwa Mohamed, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ya uhalifu.
No comments:
Post a Comment