Na Amina OMARI -Tanga
SERIKALI imesema hadi sasa kuna wagonjwa wanne tu wa corona nchi nzima.
Imesema idadi ya wagonjwa imepungua kwa kiasi kikubwa, huku mikoa ya Tanga na Mwanza ikiwa haina wagonjwa na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Taarifa hiyo ya hali ya ugonjwa huo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa mkoani Tanga.
Ummy alisema hadi sasa Mkoa wa Dar es Salaam ambao ndio uliokuwa unaongoza kwa maambukizi, vituo vilivyotengwa kwa
kuwatunza wagonjwa vimebaki na wagonjwa wanne pekee.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Hospitali ya Amana wagonjwa watatu, Mloganzila mmoja, huku Hospitali ya Kibaha mkoani Pwani, ikiwa haina mgonjwa hata mmoja.
“Kituo chetu Mwanza napenda kusema nacho hakina mgonjwa hata mmoja kwa taarifa nilizozipata leo (jana) asubuhi hii, na zile hospitali zetu za binafsi zikiwa hazina mgonjwa hata mmoja,” alisema Ummy.
Alisema kwa Mkoa wa Tanga wamelazimika kufunga vituo vyake vilivyoko katika mpaka wa Horohoro na pia Hospitali ya Wilaya Maswa kutokana na kukosa wagonjwa.
“Niendelee kuwaomba wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, bado ugonjwa upo, tuendelee kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kujilinda dhidi ya maambukizi,” alisema Ummy.
Katika hatua nyingine, Ummy alisema kuwa alipata wakati mgumu katika wizara hiyo kipindi cha uwepo wa ugonjwa huo, lakini alimshukuru Rais Dk. John Magufuli pamoja na Majaliwa namna walivyoweza kumjenga.
“Katika uwaziri wangu sijawahi kupitia kipindi kigumu kama cha corona, kwa kweli nilihenya ila nashukuru Rais Magufuli na Waziri Mkuu mlinipa nguvu, nawashukuru viongozi wa dini sala zenu na dua tumeishinda corona, tukiangalia nchi nyingine tunasema Tanzania tunashukuru Mungu,” alisema Ummy.
No comments:
Post a Comment