Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
MKUU wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Dk.Sophia Mjema amewapongeza madiwani wote, wakuu wa idara, watendaji na Mkurugenzi wa wilaya hiyo kwa utendaji kazi mzuri na ushirikiano walionesha katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli.
Pamoja na hayo amesema kwa pamoja watendaji, watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala wamefanikisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato pamoja na utoaji wa mikopo kwa wananchi.
Dk.Mjema amesema hayo leo wilayani Ilala katika kikao cha Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo ambapo amefafanua kuwa ushirikiano uliopo miongoni mwao umefanikisha kutatuliwa kwa changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi huku akielezea namna ambavyo wakati wa ziara zake za kutembelea maneo mbalimbali za Wilaya hizo zilivyoweza kuzaa matunda.
Ametumia nafasi hiyo kuzungumzia barabara mbovu katika wilaya hizo ambazo amewahakikishia madiwani kuwa fedha zipo za kutosha na barabara zote Wilaya ya Ilala zitajengwa."Chini ya Rais Dk.Magufuli maendeleo yataendelea kufanyika, kinachotakiwa ni kuendelea kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kujenga Tanzania ya uchumi wa katika kusimamia miradi yote ya maendeleo".
Awali katika kikao hicho Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala imetumia baraza hilo kuwataka wanasiasa wa vyama vya siasa kutojihusisha na vitendo vya rushwa ili kupata uongozi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mchunguzi Mwandamizi wa taasisi hiyo Elly Makala amesema kutumia rushwa ili kupata nafasi ya uongozi madhara yake ni makubwa, hivyo wanasiasa wajiepushe nayo.
"Kwa wanasiasa ambao watakwenda kufanya kampeni za kuomba kura hakikisheni hamjihusishi na vitendo vya rushwa.Fanyeni siasa zenu pamoja na kampeni kwa uwazi na kujiamini na wala hakuna sababu ya kutoa rushwa,"amesema Makala.
Pia amewataka wagombea wote kujiamini ili aweze kupatikana kiongozi bora kwa ajili ya maendeleo na kuisaidia Serikali. Aidha ametoa onyo kwa wagombea ambao watajitoa dakika za mwisho kwa ajili ya kuchukua rushwa ili asigombee nafasi yake aliyoomba ridhaa kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akimkabidhi cheti cha Shukrani Diwani wa Kata ya Kata ya Ilala Saady Kimji,vyeti hivyo vimetolewa na Mkurugenzi wa manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment