MUIGIZAJI ambaye anajinasibu kuwa ni Mlokole; Muna Alphonce, amedaiwa kulichefua kanisa kwa mambo anayoyafanya mitandaoni.Kupitia ukurasa wake wa Instagram, amekuwa akitupia vipande vya video vinavyomuonesha ‘akikata mauno kama hana akili nzuri’ jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni kulichafua kanisa kwa ujumla.
Mwenyewe amekuwa akiweka sebene analoliita ni la Yesu, lakini uchezaji wake umekuwa ukikosolewa kwani viuno anavyokata vinaweza kuwaweka mtegoni hata wachungaji, kwani mavazi yake pia si ya staha.
“Wewe angalia yeye ni kioo cha jamii, ana watu wangapi wanamuangalia nyuma yake? Anavyokata mauno na kutuonesha sehemu yake ya makalio, tena kwa nguo za kubana, anakuwa anataka nini,” alihoji mdau aliyepiga simu kwenye chumba cha habari cha RISASI MCHANGANYIKO
Gazeti hili liliingia kwenye ukurasa wake huo na kujionea video tofauti tofauti ambazo ameziposti huku akisindikiza na jumbe mbalimbali za kujihami kwa wale ambao anatarajia watamtukana.
Licha ya kutahadharisha kwamba yupo tayari kwa watu kumtukana maana anawajua tabia zao, bado wachangiaji wengi kwenye kurasa zake walimtukana matusi mazitomazito ambayo hayaandikiki gazetini.Wengi wao walisema analidhalilisha kanisa kwa kusema yeye ni Mlokole, ambapo walimshauri aache kutumia wokovu huo kwa kutenda maovu.
“Unafikiri haya makanisa yanayompokea kufanya huduma na shughuli zake mbalimbali, anayaweka kwenye nafasi gani? Vipi kuhusu wachungaji wake? Huku ni kunajisi kanisa kwa kweli. Bora uamue kubaki wa dunia tujue moja kuliko kujifanya mtumishi kumbe mnafiki,” aliandika mdau mwingine mtandaoni.
Hata hivyo, muigizaji huyo hakuonekana kujali, licha ya watu kumtukana, lakini bado amekuwa haachi, anaendelea kuposti tu video hizo.
Mwandishi Wetu, Risasi
No comments:
Post a Comment