WANYAMA 380 wamekufa kwa kugongwa na magari ndani ya mwaka mmoja 2019 katika eneo la mapito ya wanyama kuanzia Magugu wilayani Babati hadi Makuyuni wilayani Monduli ambayo husaidia wanyama kwenda hifadhi ya tarangire na hifadhi ya Manyara.
Mtafiti wa wanyamapori katika mradi wa Simba Tarangire, Dk Bernard Kissui alitoa taarifa hizo juz katika kikao cha kujadili kuokoa eneo la mapito ya wanyama kwa kuchinja hadi Mdori ambalo linaendelea kuvamiwa .
Dk Kissui alisema kati ya januari hadi Desemba 2019, wamebaini wanyama 380 kugongwa katika barabara hiyo hali ambayo inatishia uhai wa hifadhi za taifa za Tarangire na Manyara.
Alisema katika eneo hilo ,licha ya wanyama kugongwa pia kuna uvamizi mkubwa wa wananchi, kulima na kuweka makazi ndani ya eneo hilo.
“Kama serikali isipochukuwa hatua sasa, wanyama wengi watapotea lakini pia tutaathiri ikolojia ya Tarangire na Manyara”alisema
Alisema wanyama hao, wanagongwa wengi nyakati za
usiku hasa kutokana na mwendokasi ya magari.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantite Kanyasu, aliagiza Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Wanyamapori(TAWA) na Taasisi ya Utafiti wanyamapori(TAWIRI), kuandaa mabango na kuweka katika eneo la barabara hiyo kutoka Arusha hadi Babati.
“naagiza kuwekwa mabango ya kuonesha faini ukigonga mnyama mfano simba dola 4000,pia yawekwe mabango ya kupunguza mwendo kwa kuonesha wanyama wanaovuka maeneo hayo”alisema
Alisema pia atazungumza na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi,ili kuhakikisha zinawekwa alama za kupunguza mwendo za kisasa ambazo haziwezi kuisha kwa muda mfupi.
Mkurugenzi wa utafiti wa TAWIRI, Dk Julius Keyyu alisema ili kuokoa wanyama na mapito yao ni muhimu kuwepo ushirikiano baina ya wananchi, viongozi wa vijiji na wadau wa utalii.
Dk Keyyu alisema tayari taasisi kadhaa zimekuwa zikifadhili mradi wa kufatilia wanyama, ikiwepo taasisi ya Chemchem Foundation ambayo imegharamia mradi wa Tembo katika eneo hilo kufungwa vifaa vya mawasiliano kufatilia mapito yao.
Akizungumzia taaarifa hiyo,Mkurugenzi wa Wanyamapori
nchini, Dr Maurus Msuha alisema ni lazima sasa serikali kwa kushirikiana na wadau kuchukuwa hatua za kulinda eneo hilo la mapito ya wanyama.
Alisema Katika kulinda eneo hili ni lazima barabara kuwekwa alama na kutolewa adhabu kwa wanaogonga wanyama lakini pia katika kulinda mapito ya wanyama wananchi wanapaswa kushirikishwa ili kupisha maeneo ya mapito ya wanyama
No comments:
Post a Comment