Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisaini salamu za rambi rambi Kumpelekea Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kufuatia vifo vya Watanzania kadhaa Mkoani Morogogo vilivyosababishwa na mripuko wa Gari la Kubebea Mafuta.Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemtumia salamu za rambi rambi Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kufuatia vifo vya Wananchi kadhaa vilivyotokea huko Msamvu Mkoani Morogoro kufuatia ajali ya mripuko wa Gari la kubebea Mafuta ya Petroli.
Katika salamu hizo Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alisema yeye binafsi pamoja na Wananchi wa Zanzibar wamekumbwa na jitimai zito lililotokana na ajali hiyo mbaya iliyogharimu uhai wa Makumi ya Watanzania.
Alisema huo ni msiba mzito kuwahi kutokea Nchini uliowagusa Watanzania wote Bara na Zanzibar na sio kwa Wana wa Morogoro pekee. Hivyo ametumia pia salamu hizo za rambi rambi kuwapa pole Wananchi na Familia za Jamaa waliofariki kutokana na janga hilo lililosababisha Maafa.
Balozi Seif amewaombea kwa mwenyezi Muungu wale Watanzania waliopata majeraha awajalie kupona haraka ili warejee katika harakati zao za kujitafutia Maisha na Familia zao.
Balozi Seif aliwataka Wananchi wote waliokumbwa na Maafa hayo kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kizito cha msiba wa wapendwa wao.
Halkadhalika Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na Maafa Zanzibar aliwatahadharisha Wananchi wote wa Tanzania kukimbilia majanga yanayoweza kuepukika.
Ajali ya mripuko wa Moto katika gari hilo la kubebea mafuta ya Petroli Mkoani Morogoro kwa taarifa za awali inaelezwa kusababishwa na cheche za moto zilizosababishwa na Mtu aliyetaka kuiba Betri ya Gari lililopata ajali.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment