Mbunge wa Viti Maalum Taifa anayewakilisha kundi la vijana, Mhe Mariam Ditopile ametimiza ahadi aliyoitoa mbele ya Rais Dk John Magufuli alipofanya ziara wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Mhe Ditopile aliahidi kuchangia mabati 200 yenye thamani ya Sh Milioni Tano kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Sagara ambayo iliezuliwa na upepo mkali na hivyo kusababisha changamoto kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Amesema yeye kama Mbunge anayewakilisha vijana ni lazima aoneshe kwa mfano utumishi wake kwa vijana ambao aliomba ridhaa ya kuwatumikia bila kujali itikadi zao.
" Nwapongeze waalimu kwa uzalendo wenu wakuendelea kuwafundisha watoto hawa katika mazingira haya magumu naamini Mwenyezi Mungu atawalipa hapa hapa Duniani na kesho kwa namna mnavyojitoa kwa kizazi hiki ambacho ndio Taifa la kesho.
" Niwafikishie salamu za Rais Magufuli anawasalimu sana wana Sagara na naamini atakuja mwenyewe kuja kujionea ukarabati huu, pia anasema anawapenda sana," amesema Mhe Ditopile.
Aidha Mhe Ditopile ametoa salamu za Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai na kuwaeleza kuwa Mbunge wao ameshindwa kufika katika tukio hilo kutokana na kubanwa na majukumu mengine.
" Niwaase ndugu zangu sasa tutumie hichi kidogo tulichonacho mkononi mpaka kiishe ili tujue tumekwama wapi, isipokuwa ili hiki kidogo kiweze kufanya kazi kubwa niwaombe wana Sagara kama mlivyoanza muendelee hivyo hivyo kwa kujitolea nguvu kazi pamoja na mchanga na kokoto.
Pia niwakumbushe hii shule ni moja ya shule kongwe katika Mkoa wetu wa Dodoma na imetoa viongozi wengi wa serikali na nje ya serikali basi tusisite kuwashirikisha katika ukarabati huu," amesema Mbunge huyo.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Santus Haule amemshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa kwake na shida za Watanzania na kumpongeza kwa utendaji kazi wake na kuahidi kumpa kura za ndio kwa niaba ya wananchi wa Sagara ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2020.
" Tunampongeza Rais Magufuli kwa namna anavyofanya kazi, ziara yake hapa kwetu ilizaa matunda makubwa sana na sasa tunakamilisha ujenzi wetu. Tunamuahidi ushindi wa kishindo 2020," amesema Mwalimu Haule.
No comments:
Post a Comment