Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kuwa na mfumo wa utoaji vibali kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri, Dkt. Ndugulile ametoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ilipotembelea na kujifunza TMDA kuhusu mifumo ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa upande wa Bara.
Amesema mfumo wa mtandao umerahisisha wateja kuomba vibali huko waliko bila ya kufika ofisini na hivyo kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
Aidha, Dkt. Ndugulile amepongeza utayari wa TMDA katika kutoa msaada wa kiufundi kwa taasisi nyingine za kiudhibiti.
Dkt. Ndugulile amesisitiza ushirikiano kati ya TMDA na taasisi ya ZFDA ya zanzibar katika uboreshaji wa utoaji huduma bora za udhibiti wa dawa nchini.
Vilevile, Naibu Waziri ameitaka TMDA kuanza mchakato wa kufuzu ngazi ya nne ya Shirika la Afya Duniani (WHO maturity Level 4) maana vigezo na uwezo upo kutokana na kazi kubwa inayofanyika katika katika udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Amesema TMDA hivi sasa imekuwa taasisi ya kwanza Barani Afrika kufikia ngazi ya 3 ya WHO (ML3) jambo ambalo nchi inajivunia kwakuwa usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi huakikiwa ipasavyo kabla ya kumfikia mtumiaji ili kulinda afya ya jamii nchini.
Ndugulile amesisitiza kuwa dawa zote zilizo nchini kutoka ndani na nje ya nchi ni salama na hakuna dawa yenye madhara kwa binadamu.Pia amekemea matumizi mabaya ya dawa hususani vijiua sumu (antibiotic ) na kuwataka wauzaji wenye maduka ya dawa kuacha kuuza dawa bila ya cheti cha daktari.
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika ziara yao imetembelea pia maabara ya TMDA ili kujionea uwekezaji mkubwa wa mitambo iliyopo na kuona namna ya kuboresha kwa upande wa visiwani Zanzibar.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani),mara baada ya kuwapokea Wajumbe wa Kamati ya Bajeti Bunge la wawakilishi Zanzibar walipotembelea ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),leo jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment