Dr. BASHIRU ALLY KAKURWA aliteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, Mh. Dr. JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI na kisha kuidhinishwa na NEC ya CCM kuwa Katibu Mkuu wa CCM tarehe 29 Mei 2018. Zifuatazo ni nukuu za Mwanazuoni huyu nguli na Mpenda mijadala ambazo amezitoa nyakati mbalimbali akitekeleza majukumu yake mapya ndani ya CCM:
1. "Nimekuta wizi wa kutisha kwenye chama chetu na wengine nikiwataja hamtanielewa. Wanajifanya ni waheshimiwa kumbe ni wezi, wameiba magari, wameiba ardhi. Ukiwaskia nje wanabwatuka unawezakudhani ni wazalendo kumbe ni mijizi na kwenye vikao mkikaa hata kabla hamjafikia maamuzi, mijizi hiyo inatoka nje".
2. "Mijadala ndio namna ya kuendeleza nchi yetu, mijadala ndiyo inatufanya tujisahihishe. Hatuwezi kusonga mbele bila mijadala. Tumekosea sana katika nchi yetu, tumepotea sana katika nchi yetu. Mbaya zaidi tumeanza kuogopa kusema ukweli, lazma tubadilike".
3. "Tuambizane ukweli; kuanzia sasa CCM haitachukua tena wanamuziki kwaajili ya kampeni za chaguzi. Hivi wananchi mkiishapewa kofia na fulana halafu nyimbo za "mbele kwa mbele" zikapigwa, huwa mnapata nafasi ya kuhoji sifa za mnayetaka kumchagua? Wanamuziki wanakichaji chama fedha nyingi na wanafaidika wao na matumbo yao. Hivyo, kuanzia sasa hakuna tena kitu kama hicho";
4. "Wapigakura wajanja wameanza tabia ya kudharau chaguzi. Wanabaki nyumbani kwani wanaona chaguzi ni kituko, ni mchezo wa kuigiza. Ndio maana leo kupata watu wa kwenda kupiga kura imekuwa shida. Note CCM tunakoshinda ni chini ya 30%, chini ya 40% . Hakuna mahali ambako wapigakura wamejitokeza kwa 50%. Na mwaka 2010 ulitia fora. Watu wengi walijiandikisha kumbe walikuwa wanataka kile kiparata (kitambulisho cha mpigakura) kwasababu huwa kinatumika polisi kumwekea mtu dhamana. Wakiishakipata wanaingia mitini. Kwa mara ya kwanza katika historia nchini, mwaka 2010 tukapata serikali ambayo haina uhalali wa kisiasa kwasababu 50% ya wapigakura walibaki nyumbani".
5. "Msimu wa uchaguzi umekuwa msimu wa rushwa. Imefika mahali wagombea wanauza adi nyumba. Wengine wanaomba sana michango. Usipomchangia anakuwa mkali na kununua uso utadhani anakwenda kutibiwa. Akiishazikusanya fedha anakwenda kuwanunua mawakala, nao wanawanunua wananchi. Wananchi mnachotakiwa kufanya ni kubomoa soko la kura".
6. "Napenda kuwafahamisha kwamba HUSSEIN BASHE sio mkorofi bali ni miongoni mwa wabunge wa CCM wadadisi. Kuna tofauti kubwa kati ya mdadisi na mkorofi. BASHE na NAPE NNAUYE ni miongoni mwa wanachama wetu wadadisi na wanasaidia kulichangamsha bunge ila wanatofautiana katika udadisi wao. NAPE kidogo ana joto zaidi kuliko BASHE. Wote nawafahamu vizuri hivyo msidanganywe kuwa NAPE na BASHE ni watukutu. Sio watukutu, ni wadadisi na wamewezesha mawaziri kufikiri kabla ya kutenda. Kutenda kila mmoja anawezakutenda, hata mwendawazimu anaweza kutenda lakini ili uweze kutenda kwa ufanisi na tija lazma ufikiri. Michango ya BASHE bungeni inafikirisha".
7. "Mimi ninachosisitiza ni nidhamu na si kunyamazisha watu. Tutapata wapi fikra mpya bila kuhojiana, bila kujadiliana na bila kudadisi? Tusipofanya hivyo, Chama Chetu cha Mapinduzi kitakuwa chama mfu".
8. "Nilikuwa Morogoro na akatajwa Waziri kuwa anamiliki hekari 1000. Watu wanatakakujua amezipataje na mi ntamwita waziri huyo nimuulize kusudi nikawajibu walioniuliza. Hatuwezi kuwa na viongozi ndani ya chama kinachojitambulisha kama chama cha wanyonge halafu baadhi yetu tunapora ardhi ya wanyonge. Ni suala la kuchagua kati ya kuwa Kiongozi wa CCM au kuwa Mporaji wa ardhi".
9. "Na hii habari ya "Dar Es Salaam ya MAKONDA" sio sahihi. Hakuna "Dar es Salaam ya MAKONDA" ni "Dar we Salaam chini ya Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, MAKONDA". Kuna wakati huwa namsikia MAKONDA akasema "Wananchi wangu", nani kamwambia ana wananchi wake? Hakuna wananchi wako. Hakuna kiongozi anamiliki wananchi, ni "wananchi wenzangu". Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya juu ya ubinafsi .."mkianza kusema- mimi, wewe, sisi au wao hamfiki". Vongozi vijana mnapaswa kuwa wanyenyekevu na kuacha papara. Vinginevyo mtapotea kama walivyopotea viongozi wengine vijana waliopewa madaraka wakakosa unyenyekevu" .
10. "Nawashukuru sana watanzania. Nawashukuru watanzania kwa kunisomesha kwa kodi zao na hatimaye nikaweza kupata shahada zote tatu, kamwe sitawasahau watanzania. Nina deni kubwa la kulipa utumishi uliotukuka. Kazi niliyopewa ya kuwa Mtendaji Mkuu katika chama ni kubwa mno".
KWA hakika, nukuu hizi kuntu zinamtanabaisha Mh. BASHIRU kuwa ni mwanadamu wa aina gani, amedhamiria kuifanya CCM iwe chama cha aina gani na pia viongozi wa serikali ya CCM waweje.
No comments:
Post a Comment