Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
NAIBU Waziri wa Maji Juma Aweso amezitaka Mamlaka za maji nchini kuiga mfano wa DAWASA wa kuwaunganishia maji wananchi kwa mkopo na kuwakata kidogo kidogo kil mwisho wa mwezi.
Aweso ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam kwenye banda la maonesho la Mamlaka hiyo kupata maelezo mbalimbali kwenye Wiki ya Maji duniani iliyofikia kilele.
Akizungumza baada ya kumaliza kupata maelezo kuhusu huduma wanazozitoa kwenye banda la Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA , Naibu Waziri amesema kuwa maji yapo ila changamoto kubwa ni wananchi wanatakiwa kuunganishwa huduma ya maji na kikubwa DAWASA waliona umuhimu na kuwaunganishia maji wananchi na kuwakata kidogo kidogo kila mwisho mwezi.
Aweso amesema, katika wiki hii ya maji watendaji wanatakiwa wajitafakari kuanzia kwenye utendaji, changamoto na mafanikio kwenye sekta ya maji pia tutambue maji ni uhai na uchumi na tutoke maofisini tuingie mtaani kutatua changamoto za maji.
“Mamlaka zote wanahakikishe wanawaunganishia maji wananchi na waige mfano wa DAWASA wa kutoa vifaa na kuwaunganishia maji wananchi na baadae kuwakata kidogo kidogo kila mwisho wa mwezi,”amesema Aweso.
Ameeleza kuwa bado kuna changamoto za maji katika maeneo ambayo hayana mtandao kwa mkoa wa Dar es Salaam, kuna mradi wa Visima vya Kimbiji na Mpera ambapo vipo katika utekelezaji sasa nataka DAWASA waelekeze nguvu zao zote na kazi ianze mara moja ili wananchi wa Temeke, Ukonga, Kigamboni na maeneo mengine wapate maji safi na salama.
“ kuna miradi 1659 imeshakamilika, na miradi mingine 492 ikiwa ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ninaamini itakamilika kwa wakati na mwananchi anatakiwa apelekewe maji mita zisizozidi 400 kutoka mahala anapokaa,” amesema.
Aweso amezungumzia pia ujenzi wa mabwawa ya maji ambapo amesema hiyo ni fursa kwa Wizara kwani kuna maeneo yana mafuriko ikiwemo Kilosa Mkoani Morogoro na watatumia nafasi ya kujenga mabwawa wanaweza wakayatumia kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na kutatua kero ya maji Kwene Jiji la Dodoma na Morogoro ikiwemo.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Arone Joseph amesema kuwa wamefurahi kwa Naibu Waziri ambaye ni mzazi kwao kuweza kufika kwenye mabanda yao ambapo ndani ya wiki ya maji wameweza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kusikiliza kero za wananchi.
Joseph amesema, wameweza kusikiliza kero 150 za wananchi na asilimia 70 zikiwa zimefanyiwa kazi na nyingine zikiwa zinaendelea kutatuliwa.
Ameongeza, Katika moja ya mikakati yao ndani ya wiki ya maji duniani ilikuwa ni kuhakikisha wanamaliza miradi mbalimbali na wananchi waanze kupata maji na hilo limefanikiwa kwenye maeneo ya Bonyokwa, Kiwalani, Saranga, Kinzudi, Kwa Msuguri na Bagamoyo.
“Kuna miradi mingine mikubwa bado inaendelea kutekelezwa ila malengo ni kufikia asilimia 95 ya wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wanapata majisafi na Salama,” amesema Joseph.
Wiki ya Maji imefikia kilele leo ambapo kitaifa imefanyika Jijini Dodoma na malengo yakiwa ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa kwenye kupata huduma ya majisafi na kumtua mama ndoo kichwani.
Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutembelea na kupata maelezo kwenye banda la maonesho la Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA leo katika Kilele cha Wiki ya Maji kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso akizungumza na wananchi waliofika kwenye banda la maonesho la Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA leo katika Kilele cha Wiki ya Maji kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment