Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye(Mb) amelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation kuongeza juhudi katika kusambaza Huduma za Mawasiliano ili kuwafikia Wananchi wote katika pembe zote za Nchi,
Akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL katika ziara yake ya siku moja kukagua utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo, Mhe Nditiye amesema, Serikali inathamini mchango mkubwa wa Shirika hilo na inataka kuona jitihada zaidi zikichukuliwa katika kuboresha ufanisi wa Shirika na Sekta ya Mawasiliano Nchini.
“TTCL ni Shirika la Umma, Nawapongeza kwa yote mazuri mnayoyafanya na hasa kwa ubunifu wa huduma na gharama nafuu za huduma hizo kwa Wananchi, Huduma ya Video Conference imetoa matokeo mazuri sana, itaokoa muda na gharama kwa kuwawezesha Watendaji wa Serikali kuwasiliana bila kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine. Napongeza pia huduma ya malipo kwa kadi inayotarajia kuanza hivi karibuni, hizi ni juhudi ambazo Serikali inaziunga mkono.”
Pamoja na kupongeza juhudi za TTCL zilizowezesha Shirika hilo kuongeza mapato, idadi ya Wateja wake na wigo wa upatikanaji wa huduma Nchi nzima, Mhe Nditiye ametoa Siku 30 kwa Menejimenti ya Shirika hilo kuhakikisha kuwa linaondoa kero ya upatikanaji wa Vocha na Laini za simu(Simcards) katika maeneo mbalimbali Nchini.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Corporation Mhandisi Omari Nundu amesema, baada ya kufanya vyema katika mwaka 2018, TTCL imejipanga vyema kufanikisha malengo yake kwa mwaka 2019 ambapo limekusudia kuimarisha Idara na Vitengo vyake ili kuongeza viwango vya ubora wa huduma kwa Wateja sambamba na kutekeleza majukumu ya Shirika kwa Umma.
No comments:
Post a Comment