A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, September 4, 2018

HATIMAYE MAMA MJANE APATA HAKI YA MIRATHI

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema kila mtu ana haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria [Ibara 24(1)]. Haki hii inawahusu wanaume na wanawake na chini ya Sheria ya Ardhi (1999) na Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999), wanaume na wanawake wana haki sawa za kumiliki mali pia.

Mtu yeyote anaweza kuona kwamba sheria hizi mbili pamoja na Katiba zinaweka wazi kuhusu haki ya kumiliki ardhi Tanzania, lakini sivyo inavyotendeka katika sehemu mbali mbali za jamii yetu. Matukio ya mjane kupoteza haki zake za mirathi baada ya kifo cha mume wake ni tatizo sugu katika jamii nyingi hapa nchini.

Katika Mkoa wa Geita, Bi Msegena Jeremia alifiwa na mume wake mwaka 2015 na kubaki na jukumu la kulea watoto sita peke yake. Wakati akiwa bado na huzuni ya kuachwa na mume wake mpenzi, ndugu wa mume wake waliitisha kikao kwa lengo la kugawana mali iliyoachwa na mume wake bila ya kumshirikisha.

Kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la mume wake, mtoto mkubwa wa kiume ndiye anayemilikishwa mali iliyoachwa na marehemu baba yake. Mume wa Msegena alikuwa na mtoto mkubwa kwa mke mwingine anayeitwa Joshua. Huyu ndiye kikao cha wanandugu kilimfanya kuwa msimamizi wa mirathi, ambayo ilikuwa ni nyumba, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya benki na pikipiki.

Joshua alielekezwa ndugu wa baba yake kutoa fedha zilizokuwa zimewekwa benki kwenye akaunti ya baba yake, ambazo zilikuwa ni Sh1.9 milioni na kuziweka kwenye akaunti zilizofunguliwa kwa kila mdogo wake ili kupata sehemu yao ya mirathi. Nyumba na pikipiki zilipangwa kuuzwa.

Huu ulikuwa mwanzo tu wa mlolongo mzima wa matatizo ya Msegena. Kwa mshangao mkubwa, Joshua aliweka fedha zote kwenye akaunti yake binafsi na alivyoulizwa kwa nini alifanya hivyo kinyume na utaratibu wa kisheria alimshambulia Msegena na kutishia kukata mikono yake. Huku uhusiano kati ya Joshua na Msegena, ambaye ni mama yake wa kambo, ukididimia, ndugu wa mume wake Msegena walishirikiana kumfukuza aondoke nyumbani.

“Joshua alinifungia nje ya nyumba na nililala siku mbili kwa jirani bila ya kujali usalama wangu. Siku ya tatu nilikosa uvumilivu, hivyo nilienda mjini kuomba msaada sehemu ambayo ningeweza kuupata,” alisema Msegena huku machozi yakitiririka kwenye mashavu yake.

Kule mjini alibisha mlangoni kwa kila aliyemfikiria angemsaidia akiamini atafunguliwa mlango ili atue mzigo wake aliokuwa ameubeba kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa hadi polisi na kwenye Mahakama ya Mwanzo. Moja ya matukio ya kugonga kwake kwenye mwamba ni pale Joshua, ambaye sasa alikuwa na fedha nyingi aliweza kumhonga hakimu wa mahakama ambaye aliamua kesi kwa upendeleo.

Hata hivyo, si kila ndugu wa mume wa Msegena hakuguswa na changamoto alizokuwa akizipata baada ya kuachwa na mume wake mpenzi. Wifi yake Msegena alikuwa anamfahamu msaidizi wa kisheria Geita, Bw Bernard Mosira. Aliamua kumsaidia Msegena kwa kumtambulisha kwa msaidizi wa kisheria ili apate msaada zaidi. Neema ilimjia Msegena kupitia Bernard Mosira, ambaye aliamua kuwasiliana naye kwa lengo la kumsaidia.

“Nilimwita Bernard na kumwelezea tatizo langu. Alinishauri nirudi nyumbani na aliahidi kwamba atawasiliana nami ili anisaidie katika kesi hii,” alisema.

Baada ya kufika nyumbani, mwenyekiti wa kijiji aliitisha mkutano ujulikanao kwa kimila kama “Nzengo” kwa lengo la kumtenga na kumfukuza Msegena kijijini kwa madai kwamba alikuwa akijihusisha na vitendo vibaya, ambavyo kwayo hastahili aishi kijijini pale.

Baada ya kusikia habari hizi za kusikitisha, Bernard alisafiri hadi kijijini kwa Msegena siku iliyofuata na kwenda kuwaona viongozi ili apate kumsaidia Msegena kutulia tena na kuishi kwa amani huku akiendesha maisha yake na kuwaambia viongozi wa kijiji ambacho kingewapata ikiwa wangeendelea na uamuzi wao wa kumtenga Msegena kwa lengo la lengo la kumfanya akose haki zake za mirathi.

Hivyo, Bernard alitumia uzoefu wake kumwelimisha Msegena juu ya sheria, haki na wajibu wake.

Akiwa na ujasiri baada ya kupata msaada wa kisheria na yote yaliyotokea kwake kuhusiana na haki zake za miradhi aliripoti yote aliyotendewa na Joshua jinsi alivyopelekwa kituo cha polisi na kuwekwa ndani na kupelekwa Mahakama ya Mwanzo. Baada ya kusikiliza ushahidi wote, Mahakama ilitoa uamuzi uliompa ushindi na ndugu wa mume wake waliamriwa na Mahakama kutouza nyumba yake kama walivyokuwa wamepanga na Mahakama ikasema Msegena ndiye mmiliki halali wa nyumba na pikipiki.

“Wakati wa kusikiliza kesi, niliongea kama mtu anayejua sheria na watu walionisikia, hasa hakimu na polisi, walishangaa huku wakijiuliza nilipata wapi elimu ya aina ile,” alisema Msegana.

“Tunafurahi kujifunza umuhimu wa kufuata sheria na tumeenda mbele zaidi kwa kuwaalika Bernard na wenzake na wamekuja hapa kijijini mara mbili kutusaidia kuelewa masuala ya kisheria wakati wa vikao vyetu vya kawaida,” alisema mmoja wa viongozi wa kijiji.

Yaliyomkuta Msegena ni picha halisi ya namna gani msaada wa kisheria unahitajika kwa watu, ambao haki zao za kisheria zinavunjwa kwa kukosa msaada wa kisheria. Kwa msaada wa kisheria, pande mbili za mgogoro zinaweza kupatana na kuafikiana tena. Ni jambo jema kuhamasisha elimu kuhusu haki za wajane na pia kupiga vita mila na desturi kandamizi katika jamii.

Kwa sasa Msegena ni mwanamke anayejitambua na anaishi kwa uhuru huku akitambua haki zake za msingi kutokana na msaada wa kisheria alioupata. Anaendesha maisha yake kwa kufuga kuku na kulima mazao kwenye ardhi ambayo iko karibu na nyumba yake. Pikipiki, ambayo hapo awali hakuwa na matumaini ya kuipata tena, anaitumia kubebea abiria na kwa njia hiyo hujipatia fedha inayoongeza kipato chake na kumwezesha kutunza familia yake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages