Uongozi wa Klabu ya Mabingwa Watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara Young Aficans SC (Yanga) umeupeleka mbele mkutano mkuu wa wanachama wake ambao ulitakiwa kufanyika Jumapili Mei 06, 2018 na badala yake umepelekwa Juni 17 kutokana na kubanwa kwa ratiba za za ligi kuu pamoja na ile ya kimatifa.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa na kusema kabla ya mkutano huo wanachama wa timu hiyo nchi nzima wanapaswa kuweka kadi zao za benk au zile za kawaida zikiwa hai kwa maana ya kulipia ili kila mtu aweze kutumia haki ya msingi kuweza kurekebisha mapungufu ndani ya klabu kwa kuziba nafasi za viongozi zilizowazi kwa sasa.
"Sababu zilizofanya kupeleka mkutano huo mbele ni kutokana na hapa kati kulikuwa na mechi za Ligi ambazo zilikuwa karibu karibu sana na awali tulitaka tufanye mkutano Mei 05 lakini tukaletewa ratiba ya mechi na Mbao FC na baadaye ndipo tukapata ratiba ya kombe la Shirikisho hivyo tunaamini sababu hizo ni za msingi na tusingeweza kuchanganya masuala ya mkutano na mechi", amesema Mkwasa.
Kwa upande mwingine, Yanga inatarajia kushuka dimbani siku ya Jumapili Mei 6, 2018 nchini Algeria kuminyana na USM Alger kwenye mchezo wa kwanza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
No comments:
Post a Comment