Shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF jana Mei 22 limeshiriki maadhimisho ya wiki ya ubunifu yanayofanyika Costech jijini Dar es Salaam, na kutumia fursa hiyo kueleza namna wanavyotumia teknolojia na ubunifu kuleta matokeo chanya kwa ajili ya watoto wa Tanzania.
Katika maadhimisho hayo UNICEF imeelezea kuhusu miradi yake ya kiteknolojia iliyopo hapa nchini na kuonyesha ubunifu na matokeo chanya. Moja ya mradi huo ni usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao unafanyika katika mikoa kumi na moja nchini.
Mradi huo ambao unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia wakala wa usajili wa vizazi na vifo (RITA), umefadhiliwa na serikali ya Canada, UNICEF na kampuni ya mawasiliano ya Tigo.
Mradi huo umepata mafanikio makubwa na umewafikia watoto walioko vijijini ambao sasa wameweza kupata haki yao ya msingi ya utambulisho kwa kupata cheti cha kuzaliwa.
"Kupitia mradi huu watoto wengi walioko mijini na vijijini wameweza kupata fursa hii ya kuwa na cheti cha kuzaliwa katika utaratibu ambao umerahishwa na usio na malipo. Zamani mzunguko wa kupata huduma hii ulikuwa na gharama na mlolongo mrefu na ndio maana wazazi wengi walishindwa kupata haki hii." alisema Bhaskar Mishra, ofisa kutoka UNICEF.
Aidha kwa sasa huduma hii imesogezwa karibu na makazi ya watu na gharama za kupata huduma hii zimeondolewa ambapo sasa mtoto akisajiliwa anapata papohapo cheti chake cha kuzaliwa.
" lengo letu ni kuona kuwa kila mtoto anayezaliwa nchini anasajiliwa na kupata cheti chake ndani ya muda wa wiki sita tangu amezaliwa. tunatarajia kuwa mpaka mw8shoni mwa mwaka huu wa 2018 huduma hii itakuwa inatolewa katika nusu ya mikoa yote hapa nchini." Mishra aliongeza.
UNICEF imetumia maadhimisho haya kuonyesha ubunifu na teknolojia ikiwa na lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Mradi huu ambao ulianzishwa mwaka 2012 kwa majalibio katika wilaya ya Temeke jijini Da es salaam, mpaka sasa imefikia mikoa 11 na usajili umerahisishwa kwa ofisi za kata pia kuwa ni vituo rasmi vya usajili. UNICEF inahimiza wazazi wenye watoto wenye umri wa miaka mitano kuwapeleka kusajiliwa ili wapate vyeti vya kuzaliwa.
Kutokana na kutumia teknolojia za mtandao zinazotolewa na TIGO,mpaka sasa watoto milioni 2 wameshasajiliwa.
mradi huu umewezesha kurahisisha upatikanaji wa taarifa za usajili kwa kuwa kula mtoto anaposajiliwa taarifa zake zinatumwa papohapo kwenda katika kituo kikuu cha data cha serikali kupitia teknolojia ya simu ya mkononi kutoka TIGO.
No comments:
Post a Comment