Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kuboresha reli ya TAZARA nchini ili iweze kujiendesha kwa kusafirisha mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia, kuzalisha faida na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa kwa nchi mbili.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua njia ya reli ya TAZARA na miundombinu yake katika eneo la Mlimba, Morogoro hadi Makambako, Iringa lenye umbali wa kilomita 163.
Mhandisi Nditiye amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania tunafanya majukumu yetu kwa upande wetu ambapo reli ya TAZARA inaendeshwa na nchi mbili.
Ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika kununua traction motors saba zenye gharama ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kufunga kwenye injini 42 za vichwa vya treni ili kuhakikisha kuwa treni inasafiri kwa usalama na kwa uhakika kutoka eneo moja kwenda lingine bila kuharibika njiani na kuchelewesha safari za abiria au mizigo ya wateja ambapo itaboresha utendaji kazi wa TAZARA na hivyo kuongeza makusanyo ya mapato yake.
Amefafanua kuwa, fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni tatu zitatumika kukununua mtambo na vitendea kazi kwa ajili ya kiwanda cha kutengeneza kokoto cha TAZARA ambapo kokoto hizo zinatumika kuimarisha njia ya reli ya TAZARA na miundombinu yake, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuota kwa nyasi na kupunguza mtetemo wakati wa safari.
Wakati wa ziara yake, Mhandisi Nditiye amebaini wizi wa vyuma kwenye njia za reli, madaraja na miundombinu yake ambapo vinaibiwa na hivyo kuhatarisha usalama wa safari na kuharibu miundombinu hiyo. “Naitaka TAZARA mshirikiane na SUMATRA na muwe walinzi wa reli hii na miundombinu yetu”, amesema Nditiye.
Pia, ametoa rai kwa wanunuzi wa vyuma chakavu kuwa waangalifu wasinunue vyuma vya reli. Ameilekeza TAZARA kwa kutumia kitengo chake cha Polisi kufanya ziara za kushtukiza kwa wanunuzi na wafanyabiashara wa vyuma chakavu, wakibainika na kuthibitika wananunua vyuma hivyo, wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
Vile vile ameilekeza SUMATRA kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye njia ya reli ili kuhakikisha usalama wa usafiri wa njia ya reli.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAZARA, Dkt. Befram P. Kiswaga ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zitawawezesha kufanya ununuzi wa traction motors hizo na mitambo ya kiwanda cha kutengeneza kokoto ili TAZARA iweze kujiendesha kwa faida kama ilivyokuwa hapo awali badala ya kuitegemea Serikali kulipa mishahara ya wafanyakazi wake kama inavyofanyika hivi sasa.
Mkaguzi Usalama wa Reli wa SUMATRA, Mhandisi Hanya Mbawala amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa nia yao ni kulinda usalama wa usafiri wa njia ya reli ambapo ripoti ya SUMATRA ya hivi karibuni imeonesha kuwa hakuna hali hatarishi yoyote kwenye njia hiyo ambayo itazuia reli ya TAZARA kwa sasa kusafirisha abiria na mizigo. Aidha, amemhakikishia Mhandisi Nditiye kuwa, wataendelea kufanya ukaguzi huo mara kwa mara na kuielekeza TAZARA hatua stahiki za kufuata pale inapohitajika kuhusu usalama wa reli na miundombinu yake.
Reli ya TAZARA ina jumla ya kilomita 1,860 kutoka Dar es Salaam, Tanzania hadi Kapirimposhi, Zambia. Kati ya kilomita 1,860, jumla ya kilomita 975 zipo nchini Tanzania kati ya Dar es Salaam na Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia. Pia, reli ya TAZARA ina jumla ya madaraja 318 ambapo madaraja 272 yapo nchini Tanzania na 46 yapo upande wa Zambia. Aidha, ina mahandaki yapatayo 23, na 22 kati ya hayo yapo Tanzania na handaki moja lipo mpakani mwa Tanzania na Zambia na kati ya hayo, mahandaki 18 yapo katika eneo la Mlimba, Morogoro hadi Makambako, Iringa.
Kwa upande wa Tanzania, reli ya TAZARA ina daraja refu kuliko yote, daraja Na. 117 la Ruipa lililopo kati ya eneo la Mlimba na Makambako lenye urefu wa mita 502. Pia, katika eneo hilo, kuna daraja Na. 190 lenye kina kirefu cha mita 50 kwenda chini lililopo eneo la Kitete. Vile vile, kuna handaki refu kuliko mahandaki yote, handaki la Iganga lenye urefu wa mita 817. Reli ya TAZARA inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ambapo ilikamilika ujenzi wake na kuanza kutumika mwaka 1970.
No comments:
Post a Comment