Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth Magufuli ameguswa na kutoa msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwa wafungwa wa gereza la Ukonga huku akiwataka watanzania kuondokana na dhana potovu kuwa kila mfungwa alioko gerezani ni mhalifu.
Akizungumza na baadhi ya Maafisa wa Magereza waliofika ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea msaada huo kwa niaba ya wafungwa wa gereza hilo amesema ni jukumu la kila mmoja kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwemo wafungwa wa magereza.
Aidha, Mama Janeth amekabidhi mchele tani 4.8, unga wa mahindi tani 4.8, sukari tani 2.8 pamoja na tende huku akiwatakia mfungo mwema waumini wa dini ya kiislamu wote nchini na kuwataka kuliombea taifa ndani ya kipindi hiki ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Kwa upande wake, Kamishna Gaston Kalam Sanga Kaimu Mkuu wa Magereza amemshukuru Mama Janeth Magufuli kwa msaada huo na kutoa wito kwa wakuu wa magereza kunapo pelekwa msaada huo wahakikishe msaada huo uwafikie wahusika na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment